Baadhi ya wananchi mkoani Mara wameanza kujitokeza kuwapeleka watoto wao kupata chanjo ya polio, huku zoezi la utoaji chanjo kwa njia ya nyumba kwa nyumba likiendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Zoezi hilo linafanyika katika mitaa na vijiji mbalimbali ambapo wahudumu wa afya wanaendelea kuwafikia watoto ili kuhakikisha wanapatiwa kinga dhidi ya ugonjwa wa polio.

Baadhi ya wazazi waliojitokeza wamesema chanjo hiyo ni muhimu katika kulinda afya za watoto wao na kuzuia madhara ya ugonjwa huo unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu.
Hata hivyo, bado kuna changamoto ya baadhi ya wazazi kusita au kukataa kuwapeleka watoto wao kupata chanjo, hali inayotajwa kuhatarisha mafanikio ya kampeni hiyo.

Akizindua zoezi hilo kwa ngazi ya mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Dkt. Khalfan Haule kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, amewatoa hofu wananchi akisisitiza kuwa chanjo ni salama, huku akiwataka kuachana na habari za uvumi zinazopotosha. Amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mzazi yeyote atakayekwamisha au kuzuia mtoto kupata chanjo.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron Masatu, zoezi hilo linalenga kuwafikia watoto zaidi ya laki nane wenye umri chini ya miaka kumi ili kuhakikisha wanalindwa dhidi ya ugonjwa wa polio.

Kwa upande wao, wataalamu wa afya wameeleza kuwa chanjo hiyo ni salama na muhimu katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo, huku wakitoa wito kwa wazazi kushirikiana na wahudumu wa afya ili kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo kwa wakati.
Zoezi la chanjo ya Polio lililozinduliwa jana linaendelea katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mara hadi Machi 27,2026, huku serikali ikisisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii ili kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki bila kupata kinga.
Discussion
Reader comments
0 contributions