Wananchi wa Kata ya Kyamulaile, Wilaya ya Bukoba Vijijini, wameiomba Serikali kushughulikia changamoto ya mgao wa maji, ubovu wa miundombinu ya barabara pamoja na ukosefu wa mashine ya kudurufu mitihani katika Shule ya Sekondari Mashule.
Changamoto hizo zimewasilishwa na Diwani wa Kata ya Kyamulaile, Gideone Gregory, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho, akieleza kuwa mgao wa maji umekuwa ukileta adha kubwa kwa wananchi, hususan katika Zahanati ya Kyamulaile.

Gregory amesema ukosefu wa maji katika zahanati hiyo unakuwa kikwazo kwa akina mama wanaofika kupata huduma za kujifungua, hali inayohitaji hatua za haraka ili kuhakikisha huduma za afya zinatolewa katika mazingira salama.
Wananchi pia wanakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara, hasa katika kipindi cha mvua, ambapo barabara ya kutoka Katokoro kwenda Mkalama watu pamoja na vyombo vya usafiri vinashindwa kupita.

Diwani huyo pia ameomba barabara hiyo kufanyiwa matengenezo pamoja na kujengwa kwa madaraja na makalavati katika maeneo yanayokumbwa na changamoto ya maji wakati wa mvua ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Aidha, changamoto ya ukosefu wa mashine ya kudurufu mitihani katika Shule ya Sekondari Mashule pamoja na suala la barabara zimewasilishwa kwa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini, Dkt. Jasson Rweikiza, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mashule.

Dkt. Rweikiza akijibu changamoto hizo amesema, atahakikisha shule hiyo inapata mashine hiyo ndani ya miezi miwili, huku akieleza kuwa suala la ubovu wa barabara atalifikisha kwa Meneja wa TARURA Wilaya ya Bukoba kwa hatua zaidi.
Kuhusu changamoto ya maji, Dkt. Rweikiza amewasiliana na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bukoba, Mhandisi Evaristo Mugaya, ambaye amesema RUWASA ipo katika hatua ya kutafuta chanzo kingine cha maji ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo na kuhakikisha maji yanapatikana kwa kiwango cha kutosheleza katika maeneo yote ya Kata ya Kyamulaile.

Discussion
Reader comments
0 contributions