Na Daniel Gahu - Katavi.
Katika kuhakikisha Mkoa wa Katavi unatokomeza wimbi la maambukizi ya ugonjwa hatari wa Maralia, Serikali kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vyandarua vyenye dawa kimkoa, huku akiwataka wananchi kutumia vyandarua hivyo kwa usahihi ili kujikinga na ugonjwa wa malaria.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, DC Mwanga amesema jumla ya vyandarua 738,815 vimewasili mkoani Katavi kwa ajili ya kugawiwa kwa wananchi wenye uhitaji katika halmashauri zote za mkoa huo.

“Serikali imeleta jumla ya vyandarua 738,815 ambavyo vitagawiwa kwa wananchi ili kuongeza kinga dhidi ya malaria. Awali tulilenga kufikia kaya 162,930, lakini kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi, kaya 181,962 zimejitokeza kujiandikisha,” amesema DC Mwanga.
Amesema pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na malaria, mkoa wa Katavi bado unakabiliwa na changamoto ya ugonjwa huo na kwa sasa unashika nafasi ya 11 kitaifa kwa kiwango kikubwa cha maambukizi.

“Tunapaswa kuendelea kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya malaria. Wananchi watumie vyandarua hivi, lakini pia wahakikishe wanazingatia maelekezo ya wataalamu wa afya wanapopata dalili au wanapougua malaria,” amesema.
Kadhalika, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha upatikanaji wa vyandarua hivyo na kusisitiza kuwa matumizi yake ni sehemu muhimu ya kujikinga na ugonjwa huo.

Ameonya kuhusu imani potofu zinazodai kuwa vyandarua vyenye dawa vinaweza kumaliza nguvu za kiume, akieleza kuwa dhana hiyo haina ukweli na wananchi wanapaswa kuzipuuza.
“Vyandarua hivi vimetolewa kwa lengo la kulinda afya za wananchi, si kuleta madhara. Wananchi watumie bila hofu na waelewe kuwa ni kinga muhimu dhidi ya malaria,” amesema DC Mwanga.

Aidha, ameongeza kwa kusema vituo vyote vya afya mkoani Katavi vitatumika kutoa huduma ya ugawaji wa vyandarua, huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuhakikisha wanatunza mazingira.
Ametaja baadhi ya hatua za kuzuia mazalia ya mbu kuwa ni pamoja na kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama, kufyeka nyasi na kuhakikisha maeneo yanayowazunguka wananchi yanakuwa safi.

Discussion
Reader comments
0 contributions