wanufaika wa mradi wakiendelea na mafunzo(Picha na Tryphone Odace)
Wananchi wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma, wametakiwa kujiandaa mapema kwa msimu wa kilimo kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha.
Wito huo ulitolewa na Afisa Kilimo kutoka Kata ya Nyasha Maria Mwagama wakati akizungumza baada ya semina iliyofanyika katika Chuo cha Mubondo kilichopo Kata ya Ruhita Halmashauri ya Mji Kasulu.
Amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea wananchi uwezo wa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño sambamba na kuwapatia elimu kuhusu matumizi ya mbinu bora za kilimo zinazoweza kuongeza uzalishaji wa mazao.

Afisa Kilimo kutoka Kata ya Nyasha, Maria Mwagama (Picha na Tryphone Odace)
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Uwezo wa Wakulima katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Kupunguza Maafa na Majanga Wilaya ya Kasulu Mohamed Karata amesema mradi huo unalenga kuwajengea wakulima uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo ukame.
Amesema kupitia mradi huo wakulima wanapatiwa elimu kuhusu mbinu bora za kilimo pamoja na matumizi sahihi ya mbegu bora, hatua inayolenga kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Baadhi ya wanufaika wa mradi huo walisema mafunzo hayo yamewapatia elimu muhimu itakayowasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mvua za El Niño.

Wanufaika wa mradi wakiendelea na mafunzo(Picha na Tryphone Odace)
Wamesema watahakikisha wanatumia maarifa waliyoyapata katika kuboresha shughuli zao za kilimo na kuongeza uzalishaji.
Mradi huo umefikia kata 10 za Halmashauri ya Mji Kasulu na unaratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) kwa lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji, ikiwemo kilimo, sambamba na kuchangia juhudi za kupunguza ukatili wa kijinsia.
Discussion
Reader comments
0 contributions