Na Saada Almasi, Bariadi - Simiyu.
Mradi wa mabadiliko ya tabia nchi ambao unatekelezwa na serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 440 wa kupambana na changamoto ya ukosefu na upungufu wa maji safi na salama kwa kuvuta maji kutoka ziwa Viktoria unatarajiwa kukamilika katika wilaya tatu za mkoa wa Simiyu ambazo ni Busega,Bariadi na Itilima ndani ya miezi 18.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu Anamringi Macha katika kikao cha kutambulisha mradi huo kilichofanyika mjini Bariadi na kuwakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo wa vijiji,amewataka watekelezaji wa mradi huo ambao ni kampuni ya OTONDE kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

“Huu mradi umesubiriwa kwa muda mrefu na wananchi pamoja na kwamba uko katika hatua ya matumaini tuongeze kasi na tumalize ndani ya muda tuliokubaliana kwa sababu adha ambayo wanapitia wananchi ni kubwa kiasi cha serikali kuona haja ya mradi huu,” amesema RC Macha.
“Vijiji ambavyo vitapitiwa na mradi huu kilometa 12 kulia na kushoto zinatakiwa kupatiwa maji hivyo niombe tuongokane na changamoto na migongano na wanachi ,tutimize kile tulichokubaliana ,wananchi wanajua na wanafuatilia,” aliongeza RC Macha.

Mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu Silanga akiwa kati ya wahudhuriaji wa kikao hicho amesisitiza kuwa wananchi hawatokubali visingizio vya aina yoyote vitakavyo tolewa na mkandarasi huyo kwa kushindwa kumaliza mradi kwa wakati.
“Sisi wananchi tuko tayari kuupokea huu mradi na kutoa ushirikiano lakini muda wa miezi 18 ambao ni kuanzia mwezi huu Julai niwaambie hatutokubali kusikia kisingizio chochote kwa mkandarasi baada ya mradi kutokamilika kwa wakati nah ii ni kwa sababu tumechoka tunahitaji sana hayo maji,” alisema Njalu.

Kwa upande wa meneja RUWASAmkoa wa Simiyu mhandisi Emmanuel Luswetula amesema kuwa vijiji 81 ambayo vinapatikana ndani ya kilometa 12 vitapata maji ambapo vyote vinapatikana katika wilaya tatu za mkoa huku mkandarasi kutoka kampuni ya OTONDE Godlove Ngoda akiahidi wananchi kukamilisha mradi na kuukabidhi kwa wakati.
Discussion
Reader comments
0 contributions