Na Daniel Gahu - Katavi.
Katika kuimarisha Elimu kwa vitendo na kuwawezesha wanafunzi kupata uelewa mpana wa masuala mbalimbali ya kijamii na kitaaluma, wanafunzi wa Shule ya Msingi Mirumba iliyopo Halmashauri ya Mpimbwe, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, wamefanya ziara ya kujifunza katika Ofisi ya Makao Makuu ya Halmashauri hiyo pamoja na kituo cha Redio kinachomilikiwa na Halmashauri.
Ziara hiyo imefanyika kwa kuwakutanisha wanafunzi waliokuwa wameambatana na walimu wao pamoja na baadhi ya Wazazi, kwa lengo la kujifunza namna shughuli za utawala na uendeshaji wa Redio zinavyotekelezwa katika utoaji wa huduma kwa Wananchi.

Katika ziara hiyo, wanafunzi walipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe, Bi. Shamim Mwariko, ambaye aliwapongeza walimu na wazazi kwa ushirikiano wanaouonyesha katika kuwapatia wanafunzi Elimu inayozingatia nadharia na vitendo kwa pamoja.
Amesema, ziara za mafunzo katika taasisi mbalimbali zina mchango mkubwa katika kuwajengea wanafunzi uelewa wa moja kwa moja kuhusu taaluma na shughuli zinazofanyika katika Jamii, jambo linalowasaidia kuhusisha wanachojifunza darasani na mazingira halisi ya kazi.

Ameeleza kuwa kujifunza kwa vitendo kunawapa wanafunzi nafasi ya kupanua fikra, kuongeza hamasa ya kujifunza na kuwajengea uwezo wa kufikiria kuhusu malengo yao ya badae, ikiwemo uchaguzi wa taaluma na ajira wanazoweza kuzifanya wanapohitimu Masomo Yao.
Aidha, amewasisitiza wanafunzi hao kuendelea kuwa na nidhamu, heshima na maadili mema kwa jamii, sambamba na kuthamini juhudi zinazofanywa na Wazazi pamoja na walimu wao katika kuhakikisha wanapata Elimu bora. Pia ametoa wito wa kuongeza bidii katika masomo yao ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Na kwa upande wao walimu wa Shule ya Msingi Mirumba wamemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa mapokezi mazuri na ushirikiano aliouonyesha wakati wa ziara hiyo, huku wakibainisha kuwa ziara za mafunzo katika Taasisi mbalimbali ni muhimu kwa kuwa huwapa Wanafunzi maarifa ya ziada, uzoefu wa moja kwa moja na motisha ya kujifunza kwa bidii zaidi.

Discussion
Reader comments
0 contributions