Na William Bundala, Kahama - Shinyanga.
Serikali ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga imeweka mkakati wa kuwasaka wanafunzi zaidi ya elfu mbili ambao walifaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2026 lakini mpaka sasa hawajulikani walipo.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Steven Mwagala wakati akizungumza na Jambo Fm ofisi kwake baada ya kumalizika kwa kikao cha Watendaji wa kata na wenyeviti wa vijiji na mitaa yote ya manispaa ya Kahama.

“Katika manispaa yetu ya Kahama kuna watoto zaidi ya 2000 hawajaripoti shuleni,sasa leo tulikuwa tunapitia majina ya wanafunzi na shule walizopangiwa ili tuweze kuwafuatilia na kujua wako wapi,na wapo wanafunzi wazazi wao wamewapeleka shule za kulipia hao hatuna shida nao tunawatafute wale ambao hawapo kabisa shuleni,” amesema Mwagala.
Katika hatua nyingine Mwagala amesema kuwa kwa mzazi ambaye atabainika amekiuka sheria ya mtoto sura ya 13 kifungu cha 8 atachukuliwa hatua kwa mzazi huyo ambayo ni kutozwa faini au Kwenda jela miezi sita au yote kwa Pamoja.

“Sheria iko wazi kwa mzazi ambaye atazuia mtoto Kwenda shule sheria yam toto sura ya 13 kifungu cha 8 inaweka bayana kuwa endapo itabainika mzazi kamzuia mtoto Kwenda shule atatozwa faini au Kwenda jel miezi sita au adhabu zote kwa jumla.” Ameongeza Mwagala.
Kuhusu watoto wanaoacha shule wenyewe kutokana na sababu mbalimbali Mwagala amesema kuwa Manispaa ya Kahama inatumia kituo cha Makazi Salama ambayo yanasimamiwa na maafisa ustawi wa jamii na kupewa nasaha za umuhimu wa shule na mtoto anakuwa muwazi kueleza sababu zinazomsibu na Manispaa inachukua jukumu la kumsaidia changamoto yake.

“Wapo watoto wanakutana na changamoto nyingi katika masomo yao,wengine wanashawishiwa kufanya mitihani vibaya ili wafeli sasa sisi tunatumia kituo chetu cha makazi salama tunamkutanisha na maafisa ustawi wa jamii na kumpa nasaha na kutatua tatizo lake na mtoto anaendelea na masomo,” amesisitiza Mwagala.
Nao baadhi ya wadau wa elimu akiwemo Edwin Nyakanyenge na wamesema kuwa ni wakati sasa jamii kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuwasaida watoto waliokatishwa masomo kupata haki zao na kwamba jamii ya kisukuma iondokane na zana kuwa kusomesha mtoto wa kike ni kupoteza fedha.

“Wananchi washirikiane na serikali kubaini walipo hawa watoto,wengine pengine walihitaji elimu ila wameolewa kwa shinikizo la wazazi na wengine wameingizwa kwenye kilimo na biashara bila wao kupenda,na jamii yetu iondokane na zana kuwa kusomesha mtoto wa kike ni kupoteza fedha,” wamesema wadau hao.
Discussion
Reader comments
0 contributions