Jumla ya shilingi milioni 222.1 zilizotolewa na Serikali kupitia uwekezaji wa afya ya mama na mtoto kwa ajili ya upanuzi wa zahanati ya kijiji cha Kitema Kata ya Nyamunyusi Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma imesaidia kukabiliana na kero ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya .
Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Kitema pamoja na wananchi wa kijiji cha Mkieta wanaonufaika na uboreshaji huo unaohusisha ujenzi wa jengo la kujifungulia wazazi pamoja na nyumba ya watumishi katika zahanati ya kijiji cha Kitema akiwemo Bi. Koleda Magata wamesema awali wamekuwa wakipitia adha kubwa ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya tofauti na sasa ambapo huduma nyingi za kiafya wanapata kwa wakati na kuwa imekuwa mkombozi kwa wananchi wengi hasa wajawazito.

Baadhi ya akina mama wakaiwa wamefika katika zahanati hiyo kupata huduma, Picha na Tryphone Odace
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitema Bw. Abraham Ntebanyi amesema uwepo wa jengo la kliniki ya baba, mama na mtoto pamoja na upanuzi wa chumba cha kujifungulia imekuwa na mafunaa makubwa katika kupunguza adha ya wanawake wajawazito kujifungulia katika mazingira yasiyo rafiki jambo lililokuwa linahatarisha usalama wa afya ya mama na mtoto.
Aidha Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kitema Bw, Ezekiel Lawrence ameiambia Jambo Fm kuwa ujenzi wa nyumba mbili za watumishi, kliniki ya Baba, Mama na Mtoto, jengo la kujifungulia na kupanua jengo la wagonjwa wa nje (OPD) imewapa hamasa ya kufanya ikiwa ni pamoja na kuishi mazingira rafiki.

Hata hivyo Bw, Ezekiel amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Novemba 21, 2025 na umekamilika kwa asilimia 100, huku akiongeza kuwa upanuzi wa eneo la kujifungulia umechangia ongezeko la wajawazito wengi kujifungulia kituoni tofauti na awali.
Discussion
Reader comments
0 contributions