Na Daniel Gahu - Katavi.
Walimu katika Mkoa wa Katavi wanatarajiwa kunufaika na mradi mpya wa motisha unaolenga kuboresha mazingira yao ya kazi na kuongeza ubora wa elimu katika shule za sekondari.
Mradi huo unaojulikana kama "Teacher Shujaa", wenye kaulimbiu "Inua Mwalimu, Inua Elimu", umezinduliwa na Shirika la Green Leaf Organisation kwa kushirikiana na Mtandao wa Elimu Tanzania, ukiwa na lengo la kuimarisha ustawi wa walimu pamoja na kuongeza ufanisi wa ufundishaji, hususan katika maeneo ya vijijini.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 238 utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili katika Halmashauri za Wilaya ya Tanganyika na Mpimbwe, ukihusisha jumla ya shule 23 za sekondari, ambapo shule 12 zinapatikana katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Kupitia utekelezaji wake, mradi unakusudia kuongeza motisha kwa walimu, kuboresha uwezo wao wa kitaaluma na kuweka mazingira bora yatakayowezesha utoaji wa elimu wenye ubora zaidi kwa wanafunzi.
Aidha, mradi unalenga kushughulikia baadhi ya changamoto zinazoendelea kuathiri sekta ya elimu katika maeneo ya vijijini, ikiwemo upungufu wa walimu, uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, gharama za usafiri pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu ustawi wa walimu.
"Tunasisitiza ushirikiano wa wadau wote pamoja na utekelezaji unaozingatia weledi, uwajibikaji na maadili ili kuhakikisha malengo ya mradi huu yanafikiwa na kuleta matokeo chanya katika sekta ya elimu."

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu Mkoa wa Katavi, Bw. Kasara Kando Bulemo, amesema mafanikio ya mradi yatategemea ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wadau wa maendeleo, walimu na jamii kwa ujumla.
Ameongeza kuwa motisha kwa walimu ni sehemu muhimu ya kuboresha matokeo ya wanafunzi, kwani walimu wenye mazingira mazuri ya kazi huongeza ari ya kufundisha na kuinua kiwango cha taaluma shuleni.

Kwa upande wao, wadau wa elimu pamoja na wazazi wameahidi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo kwa kufuatilia maendeleo yake na kuhakikisha rasilimali zinazotolewa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Wamesema ushiriki wa jamii utakuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha mradi unaleta matokeo ya kudumu na kuboresha kiwango cha elimu katika Mkoa wa Katavi.

Naye Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanganyika, Bw. Kenneth Pesambili Simyemba, amesema mafanikio ya mradi huo yatachangiwa na ushirikiano madhubuti wa walimu, viongozi wa serikali, wazazi na wadau wa elimu.
Amesisitiza kuwa walimu wanapaswa kutumia fursa hiyo kuongeza ubunifu katika ufundishaji na kuendelea kutoa elimu yenye ubora itakayowajengea wanafunzi maarifa, ujuzi na maadili mema.

Mradi wa "Teacher Shujaa" unatarajiwa kuwa sehemu ya jitihada za kuboresha sekta ya elimu katika Mkoa wa Katavi kwa kuongeza ari ya kazi kwa walimu na hatimaye kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi pamoja na maendeleo ya elimu katika jamii.
Ni matarajio ya wadau mbalimbali kuwa utekelezaji wa mradi wa "Teacher Shujaa" utaleta mabadiliko chanya katika mazingira ya kazi ya walimu, kuongeza ubora wa ufundishaji na kuchangia maendeleo ya sekta ya elimu katika Mkoa wa Katavi na nchini kwa ujumla.
Discussion
Reader comments
0 contributions