Kinyanganyiro cha kumtafuta Mlimbwende wa Miss Shinyanga kinatarajia kufanyika Oktoba 11, 2026 katika halmashuri ya manispaa ya Kahama huku washiriki 15 wakitarajia kuchuana katika kinyanganyiro hicho.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Mratibu na mwandaaji wa mashindano hayo mkoa wa Shinyanga ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Hollsmile, Anord Bweichum amesema maandalizi yamekamilika na tayari washiriki wameanza kuwasili kwa ajili ya kuanza kambi.
“Maandalizi yote yameshakamilika na hivi ninavyoongea na nyinyi tayari washiriki wameanza kuingia kambini na baada ya mchujo tunatarajia kuwa na washiriki 15 ambao watachuana katika jukwaa moja,” amesema Bweichum.

Ameongeza kuwa mshindi atakayepatikana atakuwa na jukumu la kuutangaza mkoa wa Shinyanga, kwa kuonesha utamaduni wake, fursa za kiuchumi na maeneo mengine yanayoweza kuvutia wawekezaji na kutoa wito kwa wadau kujitokeza ili kulishika mkono jukwaa hilo kwa kusaidia udhamini ili kufanikisha.
“Mpaka sasa tunayo maombi ya washiriki 21 waliojaza fomu, lakini watakaohitajika kushiriki ni 15 pekee,Mchakato wa kupata washiriki unaanza Oktoba 4 hadi 7 na Oktoba 11 ndiyo itakuwa kilele cha kumpata Miss Shinyanga 2026,niwaombe wadau wajitokeze ili kutushika mkono kwa kuwa taasisi ya Hollsmile pekee haiwezi bila kushirikiana na wadau.” Amesema Bwenchum.
Kwa upande wake Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mwaita Mwinyimkuu amesema halmashauri hiyo itashirikiana na waandaaji kuhakikisha mchakato wa kumpata Miss Shinyanga unafanyika kwa haki na bila upendeleo na kwamba mshindi atakuwa na nafasi muhimu ya kutangaza fursa zinazopatikana mkoani Shinyanga ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali.

“Ofisi ya utamaduni Kahama ipo tayari kushirikiana na waandaaji wa jukwaa hili ili kuhakikisha Mshindi anapatikana bila upendeleo na ambaye atauwakilisha vyema mkoa wa Shinyanga katika kutangaza mambo yote yaliyopo katika mkoa wetu” Amesema MwinyiMkuu.
Mmoja wa washiriki wa Miss Shinyanga 2026, Editha Shushu amesema shindano hilo litawapa washiriki fursa ya kujuana, kubadilishana uzoefu na kutambua fursa mbalimbali zilizopo mkoani Shinyanga na kwamba atatumia nafasi hiyo kuonyesha uwezo wake na kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu fursa za kiuchumi na kiutamaduni zinazopatikana mkoani humo.
Amesema, “Jukwaa hili litatupa fursa ya kujuana Pamoja na kubadilishana uzoefu wa washiriki wengine,lakini pia litatupa nafasi ya kutambua fursa mbalimbali zilizopo mkoa wa Shinyanga.”

Discussion
Reader comments
0 contributions