Na Gideon Gregory - Dodoma.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini pamoja na waajiri wote wanaodaiwa fedha za makato ya wanachama wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS), kuhakikisha wanalipa fedha hizo haraka.
Silinde ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, leo Julai 6, 2026.
Amesema ucheleweshaji wa fedha za wanachama ni aina ya unyonyaji unaodhoofisha sekta ya ushirika na kuathiri maendeleo ya wanachama wake.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda haki za wanachama na kuhakikisha vyama vya ushirika vinabaki imara na kutoa huduma kwa wakati kwa wanachama wake.
Pia, amesema anaamini katika dhana ya ushirika kwa asilimia 100, akibainisha kuwa ushirika unahusu umoja, ushirikiano na mahusiano kati ya mtu na mtu, vikundi kwa vikundi na hata binadamu na Mungu.
"Huenda baadhi ya watu hawaamini katika ushirika, lakini kwangu ni tofauti kutokana na umuhimu wake katika kuleta mshikamano na maendeleo ya jamii," amesema.

Amefafanua kuwa ushirika una umuhimu katika makundi matatu, ambayo ni kiroho, kijamii na kiuchumi, akisisitiza kuwa jamii inapaswa kuutazama katika mtazamo chanya licha ya changamoto zinazojitokeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania, Tito Haule, ameiomba Serikali kuifanyia kazi changamoto ya upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kimkakati, akisema jambo hilo linaendelea kukwamisha maendeleo ya vyama vingi vya ushirika nchini.

Amesema upatikanaji wa masoko kwa mazao ya kimkakati kama korosho, pamba, chai na tumbaku bado ni changamoto kubwa inayokwamisha ustawi wa vyama vya ushirika na wanachama wake.
Discussion
Reader comments
0 contributions