Na Adam Msafiri - Mara.
Wakulima wa Kahawa wilayani Tarime mkoani Mara, wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuendelea kuboresha upatikanaji wa masoko na bei ya zao hilo, wakisema licha ya kunufaika na mafunzo ya kilimo bora kupitia mradi wa MELITTA, changamoto ya soko bado inaathiri kipato chao.
Wakulima hao, ambao ni sehemu ya wanufaika 300 wa mradi huo wakiwemo wanawake, wanasema mafunzo ya kanuni za kilimo bora, uvunaji na uongezaji thamani wa kahawa yameongeza uelewa wao na kuwajengea uwezo wa kuongeza ubora na tija ya mazao.

Mmoja wa wakulima hao, Nyangi Gagiri, amesema maarifa aliyoyapata yatamsaidia kuzalisha kahawa yenye ubora zaidi, lakini amesisitiza kuwa mafanikio hayo yataongeza tija zaidi endapo kutakuwa na soko la uhakika na bei zinazowalipa wakulima.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Martha Lazaro, amesema mradi wa MELITTA umelenga kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mafunzo ya kilimo bora cha kahawa pamoja na kuwawezesha vijana na wanawake kupata ujuzi wa kujiajiri.

Mbali na wakulima wa kahawa, zaidi ya vijana 100 wilayani Tarime wamepata mafunzo ya ufundi stadi kupitia VETA, ambapo wanasema yamewapa uwezo wa kujiajiri badala ya kutegemea ajira rasmi.
Baadhi ya wanufaika hao akiwemo Charles Gidion, Eliva Isaya na Debora Nyakiha wanasema ujuzi walioupata umebadili mtazamo wao kuhusu ajira na kuwapa fursa ya kujipatia kipato kupitia taaluma walizojifunza.

Akihitimisha hafla ya kufunga mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuanzisha na kuendeleza miradi inayowawezesha wananchi kiuchumi pamoja na kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali.

Mradi wa MELITTA, uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kwa ufadhili wa kampuni ya Melitta ya Ujerumani kupitia Plan International Tanzania kwa kushirikiana na Serikali, umewanufaisha mamia ya wakulima wa kahawa pamoja na vijana kupitia mafunzo ya kilimo bora na ufundi stadi.
Discussion
Reader comments
0 contributions