Wakulima wa mpunga katika Kata ya Mwamkulu, Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, wameiomba Serikali kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana karibu na eneo la Skimu ya Umwagiliaji Mwamkulu, wakisema umbali wa kuzifuata unawaongezea gharama za uzalishaji na kupunguza tija kwa mkulima.
Wakulima hao wamesema hayo wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hozza Mrindoko, katika skimu hiyo yenye thamani ya Shilingi bilioni 33.9, ambayo inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa kuwawezesha wakulima kulima mara mbili kwa mwaka.
Kwa mujibu wa wakulima, uwepo wa mradi huo tayari umeanza kuongeza uzalishaji, ambapo baadhi yao wameeleza kuwa wameongeza mavuno kutoka wastani wa magunia nane hadi kati ya magunia 20 na 28 kwa ekari moja.
Hata hivyo, pamoja na ongezeko hilo la uzalishaji, wakulima wamesema changamoto ya upatikanaji wa pembejeo karibu na maeneo yao inaweza kuwa kikwazo katika kufikia tija kubwa zaidi, kutokana na gharama wanazotumia kusafirisha pembejeo kutoka maeneo ya mbali.
Mkulima mmoja amesema kuwa Serikali ikiweka mazingira ya upatikanaji wa mbolea, mbegu na pembejeo nyingine muhimu karibu na skimu hiyo, wakulima wataweza kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza uzalishaji wa mpunga.
Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amewataka wakulima kutumia kikamilifu fursa inayotokana na skimu hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda miundombinu yake.
Mrindoko amesema mradi huo ni mali ya wananchi na unapaswa kutumiwa kuongeza tija katika kilimo, huku akiwataka wananchi kuepuka shughuli zinazoweza kuharibu miundombinu, hususan kuingiza mifugo katika maeneo ya mradi.
“Mradi huu ni kwa ajili yenu, utumieni kikamilifu ili kuongeza tija na kuleta mavuno zaidi. Lakini mna wajibu wa kulinda na kuhifadhi miundombinu hii, isichezewe wala kufanyiwa hujuma kwa namna yoyote ile,” amesema Mrindoko.
Aidha, amewataka viongozi wa Serikali za mitaa kuhakikisha ulinzi na usalama wa miundombinu hiyo, huku idara za kilimo na maafisa ugani wakitakiwa kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi bora ya maji na mbinu za kisasa za kilimo.
Mradi wa ukarabati wa Skimu ya Umwagiliaji Mwamkulu umefikia asilimia 83 ya utekelezaji na unatajwa kuwa mradi wa kwanza mkubwa wa umwagiliaji mkoani Katavi unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuwawezesha wakulima kuzalisha zaidi ya mara moja kwa mwaka.
Kwa wakulima wa Mwamkulu, uwepo wa maji ya uhakika umefungua ukurasa mpya katika kilimo cha mpunga. Sasa wanataka hatua inayofuata iwe ni kuhakikisha pembejeo zinapatikana karibu, kwa wakati na kwa gharama nafuu, ili uwekezaji wa Shilingi bilioni 33.9 ubadilike kuwa mavuno makubwa na kipato zaidi kwa mkulima.
Discussion
Reader comments
0 contributions