Na Saada Almasi, Meatu - Simiyu.
Wakulima wa mazao ya alizeti na mtama wilayani Meatu mkoani Simiyu wametakiwa kubadili mbinu zao za kilimo hasa katika uvunaji kwa lengo lakudhibiti kiwango cha mazao ambayo hupotea wakati huo hadi kufikisha sokoni ili kuendelea kulinda uchumi wao na kujinufaisha kibiashara.
Wito huo unafuatia baada ya wakulima wengi kupoteza zaidi ya asilimia 15 ya mazao yao kila msimu kiasi ambacho kingeuzwa kingeongeza kipato kwa mkulima.
Kufuatia hali hiyo wakulima wawezeshaji zaidi ya 40 kutoka katika vijiji 21 vya wilaya ya Meatu wamepigwa msasa juu ya namna ya kuwafikia wakulima na kuwaelimisha namna bora ya upandaji ,uvunaji na utunzaji wa mazao ili kunusuru uchumi wao.

Afisa Mradi wa Vijana Kilimo Biashara unaotekelezwa na BRAC Maendeleo Tanzania Edvita Machumu ambao ndiyo watekelezaji wa mafunzo hayo amesema kuwa mkulima kwa kutokujua huanza kupoteza kiasi kukubwa cha mazao shambani na baada ya kufikisha nyumbani hadi sehemu ya biashara hivyo wakipata watu wanaotoka jamii yao ni rahisi kuwafikia na kuwaelimisha.
“Zaidi ya asilimia 15 mazao ya mkulima hupotea,unakuta amevuna lakini pale shambani mazao yamemwagika atasafirisha kwa mkokoteni atamwaga njiani akifika nyumbani ataweka kwenye chumba ambacho kuna mazao mchanganyiko yatamwagika siku ya kuuza atafika sikoni na kuacha kiasi kikubwa chini ambacho hakiuziki hiyo ni hasara kwake,” amesema Edvita.
“tunaamini hawa wakulima wawezeshaji kwa kuwa tunawasisitiza hadi kuwa na mashamba darasa,kutumia pembejeo bora za kilimo watakuwa mfano na watawafikia wakulima hawa kuwapa elimu sahihi ili waone faida ya jasho lao na walifurahie maana watazidi kukua kiuchumi”ameaongeza Edvita

Baadhi ya washirikiwa mafunzo hayo wameiambia Jambo FM kuwa kinachochangia hasara hizo kwa mkulima ni elimu sahihi ya kutokujua ni muda gani wa kupanda na kuvuna mazao yake wengi wanafanya kwa uzoefu na marejeo ya babu yake alikuwa akifanya nini bila kujua zama zinabadilika.
“Mvua ndiyo kiashiria cha mkulima kuandaa na kupanda shamba lake lakini anapanda kwa mazoea tu bila elimu sahihi kuna mbegu zingine zitapotea tu hazita zaa,bado atavuna wakati mazao yakiwa hayaja komaa kwa hiyo mbegu zinakuwa hazijabeba kitu ama yamekomaa kupita kiasi,"
"Mfano alizeti ule muda tu wa kuvuna anakata kwa kisu huanza kupukutika,baadae mkokoteni wenye matundu ndio utapeleka nyumbani hadi muda wa kupukuchua na kuipakia kwenye mifuko kiwango fulani kinakuwa kimepotea,” amesema Anisia Mwandu, mkulima mwezeshaji kutoka kijiji cha Itinje.

Peter Laurent Magembe mwezeshaji wa semina hiyo anasema kuwa ipo haja ya serikali utenga maeneo maalum ya maghala ya mtama na alizeti kama ilivyo katiza zao la pamba ili kumsaidia mkulima kupata sehemu sahihi ya kutunzia mazao yake.
“tuangalie mkulima anatunza wapi huko nyumbani anaweka mazao aina ngapi aliyolima,kitendo cha kuchanganya zao zaidi ya moja ni upotevu tosha zile mbegu zikichanganyika pamoja si wote wataokota moja moja kuzirudisha lakini kukiwa na maghala kila kijiji mkulima anapeleka kumsubiri mnunuzi itasaidia hata kupata bei ya uhakika na kumpunguzia hasara mkulima”amesema mwezeshaji Petter Laurent
Mradi wa Vijana Kilimo Biashara unatarajiwa kuwafikia vijana wakulima wawezeshaji zaidi ya elfu 15 katika wilaya ya Maswa na Meatu huku asilimia 70 kati yao wakiwa vijana wa kike ambao mara nyingi hubaki nyuma katika suala la uzalishaji na kulinda mnyororo wa thamani ya mazao.
Discussion
Reader comments
0 contributions