Na Ibrahim Rojala, Mbogwe - Geita.
Wakulima wa Kata ya Ilolangulu Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, wameiomba Serikali kuanzisha vituo vya ununuzi wa mazao na kujenga maghala ya kuhifadhia mazao, ili kuwaepusha na changamoto ya wafanyabiashara wanaokwenda kununua mazao moja kwa moja mashambani kwa kutumia vipimo visivyo rasmi.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima hao, Simon Samike amesema uwepo wa vituo rasmi vya ununuzi wa mazao utasaidia kuondoa unyonyaji unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaofika vijijini na kununua mazao kwa bei na vipimo visivyozingatia taratibu.

‘Naiomba serikali ijenge maghala kila kijiji,wawe wanauzia pale,serikali iwe inanunua hayo mazao kwasababu wakulima wananyanyasika sana’ameeleza Samike.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Wakili Edwin Bayona amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto hiyo ikiwemo wafanyabiashara kutumia vipimo vyao wenyewe wakati wa ununuzi wa mazao nakwamba Halmashauri imeendelea kufanya doria katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wanunuzi na walanguzi wa mazao wanafuata sheria.

‘Kunakuwa na suala la lumbesa tunalizuia lakini vile vile tunakuwa tunafanya Patrol,kumekuwa na gari la halmashauri wananchi wamekuwa wakiliona linapita kuhakikisha wale walanguzi hawabebi magunia kwa kutumia lumbesalakini mheshimiwa mwenyekiti kuhusiana na maghala kwanza tunawahimiza wananchi watengeneze maghala’amesema Wakili Edwin.
Aidha ameeleza kuwa licha ya uwepo wa maghala yaliyojengwa kupitia miradi ya kilimo lakini maghala hayo yamekuwa hayatumiki kutokana na mwamko mdogo wa wananchi kuhusiana na matumizi ya maghala hayo.

Kufuatia hatua hiyo, Mku wa Mkoa wa Geita, Shigela amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani Mbogwe kuhakikisha wanatenga na kuanzisha vituo rasmi vya ununuzi wa mazao katika maeneo yao hatua hiyo itawazuia wanunuzi kwenda kununua mazao moja kwa moja mashambani.
"Muanze kutambua katika kila kijiji kituo cha kuuzia mazao ili mnunuzi asiende shambani, mkulima azalishe alete hapa,na hata kama ataamua kwenda shambani akamsaidie mkulima kusomba na kuleta kwenye soko lakini lazima aje apime kwasababu vile vile ndio halmashauri inapata mapato yake kwenye yale mauzo,’ ameagiza RC Shigela.
Discussion
Reader comments
0 contributions