Baadhi ya wakulima mkoani Mara wameiomba serikali kuongeza udhibiti dhidi ya wanunuzi wa mazao wanaotumia mizani za zamani na isiyo sahihi, wakidai hali hiyo imekuwa ikiwasababishia hasara kubwa na kudhoofisha uchumi wao.
Wakulima hao wanaohusika na uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo pamba, dengu, kahawa, choroko pamoja na tumbaku, wamesema kwamba changamoto ya kuibiwa kilo kupitia mizani imeendelea kuwa kero kwa muda mrefu katika maeneo mengi ya ununuzi wa mazao hayo.

Wakizungumza na Tovuti hii baada ya jukwaa la ushirika mkoani Mara, baadhi yao wamesema matumizi ya mizani ya kidigitali yanaweza kuwa suluhisho la changamoto hiyo kwa kuwa yataongeza uwazi na usahihi katika vipimo vya mazao yao.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa zao la pamba mkoani Mara, Fikiri Maregesi, amesema matumizi ya teknolojia katika mifumo ya vipimo yanaweza kusaidia kulinda maslahi ya wakulima na kuongeza uaminifu katika biashara ya mazao.

Aidha, baadhi ya makampuni na taasisi zinazoshiriki katika sekta ya ushirika zimesema tayari zimeanza kuhamasisha matumizi ya mizani ya kidigitali ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wakulima na kuongeza usahihi wa vipimo.
Wakati huo huo, viongozi wa vyama vya ushirika pamoja na wakulima wamekumbushwa umuhimu wa kutumia taasisi rasmi za kifedha na kuzingatia matumizi sahihi ya TEHAMA katika usimamizi wa shughuli za AMCOS, hatua inayotajwa kusaidia kuongeza uwazi na ufanisi katika sekta ya ushirika.

Discussion
Reader comments
0 contributions