Skip to main content

WAKIMBIZI WESTERN WATII AGIZO LA SERIKALI, WAHAMIA IGALUKILO

Na Daniel Gahu - Katavi.

WAKIMBIZI WESTERN WATII AGIZO LA SERIKALI, WAHAMIA IGALUKILO

Na Daniel Gahu - Katavi.

Kufuatia agizo la Serikali la kuwataka wananchi wa eneo la Western, Kitongoji cha Luhafwe katika Kijiji cha Vikonge, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, wameungana na Serikali katika uzinduzi rasmi wa zoezi la kuhamisha kaya 648 kutoka maeneo yasiyo rasmi kwenda eneo salama la Igalukilo kwa lengo la kuboresha makazi na huduma za kijamii.

Uzinduzi wa zoezi hilo umefanyika na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, akiwa ameambatana na kamati mbalimbali za utekelezaji wa zoezi hilo, ambapo amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati na kwa mafanikio yaliyokusudiwa.

“Niwaombe wananchi tuendelee kuungana katika kutekeleza maelekezo ya Serikali yaliyotolewa na Baraza la Mawaziri. Leo tunazindua rasmi mpango wa kuwapanga vizuri wananchi wanaoishi katika maeneo ya uwekezaji yasiyo rasmi na kuwapeleka katika maeneo ambayo kisheria yatakuwa mali yao,” amesema Mhe. Buswelu.

Aidha, amesema Serikali tayari imeweka miundombinu muhimu katika eneo la Igalukilo ili kuwezesha wananchi hao kuishi katika mazingira bora zaidi, huku akieleza kuwa kila kaya itapatiwa ekari sita za ardhi ya kilimo pamoja na kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa makazi mapya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Ndg. Shabani J. Juma, amesema Halmashauri imejipanga kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinapatikana katika eneo hilo ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati pamoja na miundombinu mingine muhimu kwa ustawi wa wananchi watakaohamia eneo hilo.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Luhafwe Emmanuel Kasuku Bilagi amesema kuwa ili kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa zoezi hilo, yeye atakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuhamia katika eneo jipya la Igalukilo mara baada ya kukabidhiwa hatimiliki ya eneo lake.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.