Na Daniel Gahu - Katavi.
Serikali Mkoa wa Katavi kupitia kwa Mkuu wa Mkoa huo, Mwanamvua Hoza Mrindoko, ametangaza rasmi kuanza kwa zoezi la uhamishaji wa wananchi wanaoishi katika eneo la Western–Luhafwe kwenda Igalukilo kuanzia Mei 25, 2026, katika hatua inayotekeleza mpango wa Serikali wa upangaji na matumizi bora ya ardhi kwa shughuli za maendeleo na uwekezaji mkoani humo.
Akizungumza mbele ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo hilo, RC Mrindoko amesema Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa makazi yaliyopo Western hayana uhalali wa kisheria, hali inayokwamisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo iliyokusudiwa kufanyika katika eneo hilo.

Amesema zoezi la uandikishaji wa wananchi litafanyika kuanzia Mei 25, 2026, kabla ya kuanza rasmi kwa uhamaji tarehe 27 Mei, 2026, chini ya usimamizi wa Serikali na mamlaka husika ili kuhakikisha wananchi wote wanahamishwa kwa utaratibu na usalama.
“Serikali imeandaa maeneo yaliyopimwa rasmi huko Igalukilo, ambapo kila kaya itapatiwa shamba na viwanja vyenye hati miliki pamoja na huduma muhimu za kijamii kama maji, shule, umeme na huduma za afya,” amesema Mrindoko.

Aidha, amewataka wananchi kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa zoezi hilo pamoja na kuvuna mazao yao yaliyopo mashambani kabla ya kuhamia eneo jipya ili kuepuka hasara zisizo za lazima.
Sambamba na hilo, Serikali imezielekeza Halmashauri husika kwa kushirikiana na TANROADS kuhakikisha huduma za muda za afya, ikiwemo kliniki na zahanati ya dharura, zinapatikana katika eneo la Luhafwe wakati maandalizi ya makazi mapya yakiendelea.

Wakizungumza baada ya ziara ya mkuu wa Mkoa katika makazi yao, wananchi wamesema wao wako tayari kuhamia katika makazi mapya ili kupisha uendelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali katika eneo hilo huku wakiiomba Serikali kuweka usimamizi madhubuti katika ugawaji wa viwanja ambavyo wameahidiwa pamoja na kupatiwa huduma kwa haraka ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika pale ambapo huduma hizo muhimu zitakapopatikana.
Discussion
Reader comments
0 contributions