Skip to main content

WAKAZI ZAIDI YA 13,000 MBIONI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA RORYA

Na Adam Msafiri - Mara.

WAKAZI ZAIDI YA 13,000 MBIONI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA RORYA

Na Adam Msafiri - Mara.

Zaidi ya wakazi 13,000 wa Kata ya Kyang’ombe wilayani Rorya mkoani Mara wanatarajia kupata huduma bora za afya kufuatia ujenzi wa Kituo cha Afya Ruhu, mradi unaolenga kupunguza adha ya wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Wananchi wa kata hiyo wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupata huduma za afya ngazi ya kituo cha afya, hali iliyowalazimu kwenda Kituo cha Afya Kinesi kwa gharama kubwa za usafiri na wakati mwingine kuhatarisha maisha ya wagonjwa, hususan wajawazito, watoto na wagonjwa wa dharura.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo mbele ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara iliyokuwa ikikagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ruhu, Christina Mwendwa, amesema ujenzi wa kituo hicho unaendelea vizuri na unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kata ya Kyang’ombe na maeneo jirani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, amepongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo na kuwataka wasimamizi kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zinazotarajiwa kutolewa.

Baada ya ukaguzi wa mradi wa kituo cha afya, Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mara ilihitimisha ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kwa kukagua ujenzi wa Daraja la Nyathorogo. Kamati hiyo iliipongeza halmashauri pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi.

Mradi wa Kituo cha Afya Ruhu ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa na serikali kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuwasogezea wananchi huduma muhimu karibu na maeneo yao.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.