Mahafali ya 47 hatua ya pili katika chuo cha ufundi Stadi VETA mkoani Shinyanga yamefanika na kufana huku wahitimu wakitakiwa kwenda kuwa chachu katika jamii katika kutumia ujuzi walioupata chuoni hapo kujiajiri, kuajiriwa pamoja na kuwaajiri wengine

MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA WAKILI JULIUS MTATIRO
Mahafali hayo yamefanyika leo Oktoba 23,2026 chuoni hapo ambapo mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro.
Awali akisoma Risala ya wanafunzi mhitimu Joshua Mayunga, ambaye pia alikuwa katibu wa serikali ya wanafunzi amesema licha ya kupata ujuzi chuoni hapo na kuweza hata kujiajiri wenyewe, lakini changamoto kubwa wanakwenda kukabiliana nayo ni ukosefu wa mitaji.

MHITIMU JOSHUA MAYUNGA AKISOMA RISALA KATIKA MAHAFALI HAYO
Amesema ,kutokana na changamoto hiyo wanaiomba serikali na taasisi za kifedha wawe wanafika katika chuo hicho kwa ajili ya kutoa elimu ya upatikanaji wa mikopo ili wanafunzi waweze kutambua fursa mbalimbali zilizopo.
“Licha ya ujuzi tulioupata hapa chuoni ndugu mgeni rasmi tunakwenda huko mitaani kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa ajiri ya kujiajiri wenyewe,” amesema Mayunga.

Aidha, amesema katika mahafali hayo wamehitimu jumla ya wanafunzi 234 wavulana 174 na wasichana 60, na kwamba wakati wanaanza masomo Januari 13,2025 walianza wakiwa wanafunzi 252 wavulana 187 na wasichana 65, lakini kutokana na matumizi ya dawa za kulevya wizi, ujauzito na matatizo ya kifamilia wanafunzi 18 wameshindwa kuhitimu masomo yao.

MKUU WA CHUO CHA VETA SHINYANGA THEOPHAN SEVELIN
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga Theophan Sevelin, amesema chuo hicho kimekuwa kikifanya vizuri katika kutoa mafunzo kwa vijana, ambao baadhi yao wameweza kutumia ujuzi wanaoupata kujiajiri na kutoa ajira kwa wengine.
Aidha, ameiomba serikali kuwasaidia kutatua tatizo la ukosefu wa uzio katika chuo hicho ambalo limekuwa tatizo na kutishia usalama kwa wanafunzi na mali za chuo.

Naye mgeni rasmi katika mahafali hayo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amewataka wahitimu hao kuacha kulalamikia ukosefu wa mitaji, akiwataka kutumia ujuzi walionao na kufanya kazi mbalimbali, ikiwamo vibarua, ili kujipatia mitaji hiyo na kuanzisha shughuli zao binafsi.
Amesema wahitimu wanapaswa kuacha tabia ya kujitengenezea hadhi na kubagua kazi wanazoweza kufanya, badala yake wawe tayari kufanya kazi yoyote halali itakayowasaidia kujikwamua kiuchumi wanapojitafuta kimaisha.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi maalumu, Mtatiro amesema vijana na wanawake wanayo fursa ya kuomba mikopo hiyo kwa kujiunga katika vikundi vinavyokidhi vigezo, huku watu wenye ulemavu wakinufaika na mgao wa asilimia mbili.
Amewataka wahitimu ambao hawatapata mikopo hiyo kutokata tamaa, akisisitiza kuwa ujuzi walioupata chuoni ni mtaji muhimu unaoweza kuwawezesha kujiajiri na kujipatia kipato.

Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga kimekuwa nafasi muhimu katika kuwawezesha vijana na wananchi kupata ujuzi wa ufundi unaoweza kuwasaidia kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali za uchumi.

Kupitia mafunzo ya ufundi stadi, wanafunzi wamekuwa wakipata maarifa ya nadharia na vitendo yanayolenga kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo ya jamii.

Chuo hicho kimekuwa kikitoa mafunzo katika fani mbalimbali zikiwemo umeme, uashi, useremala, ushonaji, uchomeleaji, ufundi magari , TEHAMA,pamoja na uendeshaji wa mitambo mikubwa. Aidha, kinaendelea kupanua fursa za mafunzo ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwawezesha kutumia ujuzi wanaoupata katika kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Discussion
Reader comments
0 contributions