Skip to main content

WAHIMIZWA KUZINGATIA USAFI WA KINYWA, MENO KUIMARISHA AFYA

Na Adam Msafiri - Mara.

WAHIMIZWA KUZINGATIA USAFI WA KINYWA, MENO KUIMARISHA AFYA

Na Adam Msafiri - Mara.

Wataalamu wa afya ya kinywa na meno mkoani Mara wameitaka jamii kuzingatia usafi wa kinywa na meno, wakionya kuwa kupuuzwa kwa afya ya kinywa kunachangia ongezeko la matatizo ya kuoza na kung'oka kwa meno, huku watoto na vijana wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi na uchimbaji madini wakitajwa kuwa miongoni mwa walio kwenye hatari kubwa.

Akizungumza na Tovuti hii mjini Musoma, Mtaalamu wa Afya ya Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Royal Polyclinic, Dkt. Emmanuel Sanga, amesema mazingira ya kazi yanayowafanya baadhi ya watu kukaa muda mrefu bila kufanya usafi wa kinywa baada ya kula, pamoja na kutokuzingatia matumizi sahihi ya mswaki, huchangia kuongezeka kwa magonjwa ya meno na fizi ambayo baadaye husababisha meno kung'oka mapema.

Mtaalamu wa Afya ya Kinywa na Meno kutoka Hospitali ya Royal Polyclinic, Dkt. Emmanuel Sanga.

Amesema watoto na vijana wanaofanya shughuli za uvuvi na migodini mara nyingi hukabiliwa na changamoto ya kutotenga muda wa kutunza afya ya kinywa kutokana na mazingira ya kazi, jambo linaloongeza uwezekano wa kupata matatizo ya meno.

Dkt. Sanga amesisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kupiga mswaki angalau mara mbili kwa siku, kupunguza matumizi ya vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi, hususan vinavyoshikamana kwenye meno, pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa afya ya kinywa na meno mara kwa mara ili matatizo yabainike mapema na kutibiwa kabla hayajawa makubwa.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Royal Polyclinic Musoma, Bi. Stella Eyembe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Royal Polyclinic Musoma, Bi. Stella Eyembe, amesema sekta binafsi inaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, ikiwemo huduma za afya ya kinywa na meno, ili wananchi wapate matibabu na elimu ya kinga kwa wakati.

Ameeleza kuwa uwekezaji unaoendelea katika sekta ya afya unalenga kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu karibu na maeneo wanayoishi, huku akiwahimiza wananchi kutumia huduma za uchunguzi wa afya ya kinywa mara kwa mara badala ya kusubiri mpaka wanapopata maumivu makali.

Wataalamu wa afya wanaendelea kusisitiza kuwa kinga ndiyo njia bora ya kukabiliana na magonjwa ya meno, wakibainisha kuwa usafi wa kinywa unaotekelezwa kwa usahihi unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kuoza kwa meno, magonjwa ya fizi na kung'oka kwa meno mapema.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.