Wakulima Mkoani Kigoma wameaswa kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake kujikita katika kilimo cha kibiashara kwa kuzingatia mbinu bora za uzalishaji na kuchagua mazao yenye soko la uhakika ili kuongeza tija na kipato.
Wito huo ulitolewa na Afisa Maendeleo ya Biashara kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Makao Makuu, Bi. Angelina Nyansambo, wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyowakutanisha washiriki zaidi ya 100 kutoka vikundi mbalimbali vya wakulima Wilayani Kigoma.

Afisa Maendeleo ya Biashara kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Makao Makuu, Bi. Angelina Nyansambo, Picha na Tryphone Odace
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Bi. Nyansambo alisema wakulima wanapaswa kuzingatia mbinu bora za kilimo zinazokidhi mahitaji ya soko na kuvutia wateja ili kuhakikisha wanapata tija katika shughuli zao za uzalishaji.
Naye Afisa Maendeleo ya biashara wa TADB Mkoa wa Kigoma, Bw. Patrick Kapungu, alisema mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha wakulima kupata elimu ya matumizi sahihi ya mikopo inayotolewa na benki hiyo, ili iweze kuwasaidia kukuza shughuli zao za kilimo na kuongeza uzalishaji.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuridhishwa na elimu na mbinu walizopatiwa, walisema wanaamini zitawasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo, kuongeza uzalishaji na hatimaye kuinua kipato chao.

Baadhi ya wawakilishi wa vikundi vya wakulima wakatika semina iliyoandaliwa na benki ya Kilimo, Picha na Tryphone Odace
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Benki ya TADB kuwawezesha wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo kupata ujuzi unaohitajika ili kuwa tayari kukopesheka, kutumia mikopo kwa tija na kuendeleza kilimo cha kibiashara nchini.
Discussion
Reader comments
0 contributions