Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu Balozi Simon Nyakoro Sirro amewahimiza wakulima, wafugaji, wavuvi na wafugaji nyuki katika mikoa ya Tabora na Kigoma kutumia teknolojia za kisasa kuongeza tija na kuzalisha kulingana na mahitaji ya soko.
Balozi Sirro amesema hayo wakati wa ufunguzi wa maonesho ya wakulima 'Nanenane' yanayofanyika katika Viwanja vya Nanenane Ipuli mkoani Tabora, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050.”

Maonesho hayo yamewakutanisha wazalishaji, watafiti, wataalamu, taasisi za Serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wafanyabiashara wa pembejeo na zana za uzalishaji.
Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora, Ndugu Mohamed Katete, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Pia amewapongeza viongozi na wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa miradi hiyo mkoani Tabora.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt. John Rogath Mboya, amesema maonesho hayo yanalenga kutoa elimu kuhusu mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na ufugaji nyuki pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa.

Amesema pia yanalenga kukuza biashara, uwekezaji, ushirika na upatikanaji wa masoko kwa kuwaunganisha wazalishaji na watafiti, wataalamu pamoja na sekta binafsi.
Akizungumza baada ya kufungua maonesho hayo, Balozi Sirro amewataka wazalishaji kutumia maarifa na teknolojia zinazopatikana katika maonesho kuongeza tija, ubora na thamani ya bidhaa zao.

Pia amezitaka halmashauri kutenga bajeti ya kujenga mabanda ya kudumu Ipuli na kuendeleza mkakati wa kuufanya uwanja huo kuwa Kituo Mahiri cha Ushirika, Ubunifu na Teknolojia kitakachotumika mwaka mzima kwa mafunzo, utafiti, biashara na uwekezaji.

Discussion
Reader comments
0 contributions