Skip to main content

WADAU WAPITISHA BEI MPYA ZA MAJI SHINYANGA

Na Eunice Kanumba - Shinyanga.

WADAU WAPITISHA BEI MPYA ZA MAJI SHINYANGA

Na Eunice Kanumba - Shinyanga.

Wadau wa sekta ya maji katika Mkoa wa Shinyanga wamepitisha na kuidhinisha mapendekezo ya marekebisho ya bei za huduma za maji safi na usafi wa mazingira yaliyowasilishwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha utekelezaji wa mabadiliko hayo unafanyika kwa uelewa na ushirikiano wa jamii.

Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha wadau kilichofanyika Juni 2, 2026 katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, kikihusisha viongozi wa serikali, vyama vya siasa, madiwani, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi.

Akiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya bei, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa SHUWASA, Reuben Mwandumbya, amesema hatua hiyo inalenga kuiwezesha mamlaka kuendelea kutoa huduma bora, salama na endelevu kwa wananchi huku ikikabiliana na changamoto za ongezeko la gharama za uendeshaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira.

Ameeleza kuwa marekebisho hayo yatasaidia kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama, kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa maji, kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wateja pamoja na kuwezesha utekelezaji wa miradi mipya ya upanuzi wa huduma katika maeneo mbalimbali yanayohudumiwa na SHUWASA.

"Kwa mujibu wa viwango vipya vitakavyoanza kutumika katika mwaka wa fedha 2026/27, wateja wa majumbani wanaotumia zaidi ya mita za ujazo tano kwa mwezi watalipa Shilingi 1,840 kwa mita ya ujazo kutoka Shilingi 1,740 za sasa.

Taasisi mbalimbali zitalipa Shilingi 3,060 kwa mita ya ujazo kutoka Shilingi 2,760, huku wateja wa sekta ya biashara wakiongezeka kutoka Shilingi 2,790 hadi Shilingi 3,100 kwa mita ya ujazo," ameeleza Mwandumbya.

Aidha, amebainisha kuwa, gharama za huduma ya maji kwa viwanda zimeongezeka kutoka Shilingi 2,850 hadi Shilingi 3,160 kwa mita ya ujazo, wakati viwanda vya vinywaji vitatozwa Shilingi 4,160 kutoka Shilingi 3,750 za awali. Kwa upande wa vibanda vya kuuza maji, (MAGATI)  kiwango kipya kitakuwa Shilingi 1,670 kwa mita ya ujazo kutoka Shilingi 1,500 zilizokuwa zinatumika hapo awali.

Awali akitoa taarifa juu ya mabadiliko ya bei hizo mkurugenzi mtendaji wa SHUWASA Yusuph Katpola   amesema bei zinazotumika kwa sasa zimekuwa ni za muda mrefu haziendani na gharama halisi za uendeshaji wa huduma.

Amesema  mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma za maji katika Manispaa ya Shinyanga pamoja na maeneo ya Tinde, Didia na Iselamagazi huku ikiendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma huku akiwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa bei hizo mpya ili mamlaka hiyo iweze kutekeleza majukumu yake  kwa weledi.

Naye  Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya SHUWASA, Reuben Kitinya, amesema mabadiliko hayo yametokana na kupanda kwa gharama za mabomba, viungio, madawa ya kutibu maji, vifaa vya uendeshaji na matengenezo ya miundombinu ya maji pamoja na mahitaji yanayoongezeka ya wananchi ya kupata huduma bora.

Amesema lengo la marekebisho hayo si kuwaongezea wananchi mzigo usio wa lazima, bali kuiwezesha SHUWASA kuendelea kutoa huduma endelevu, salama na yenye ubora unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Mgeni rasmi katka kikao hicho ambaye ni  Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro,  ameipongeza SHUWASA kwa juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma za maji na kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi inapaswa kuendelea kutolewa kwa nguvu kubwa ili jamii ielewe sababu za mabadiliko hayo na manufaa yatakayopatikana.

Bei hizo mpya zinatarajiwa kuanza kutumika kuanzia tarehe 1 july  2026

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.