Na Adam Msafiri - Mara.
Wabunge wa mkoa wa Mara wamepatiwa mifuko 6,000 ya saruji kupitia Taasisi ya Nyansaho Foundation, ili kusaidia ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya, hatua inayolenga kuboresha huduma na kuleta nafuu kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho amesema, msaada huo unalenga kuchochea maendeleo ya miundombinu huku akihimiza kuanzishwa kwa mkakati wa kimkoa wa kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Nao Uongozi wa mkoa wa Mara, umekaribisha jitihada zaidi za wadau wa maendeleo ndani na nje ya mkoa, ili kuunga mkono serikali katika kuboresha miundombinu.
Mkuu wa mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amepongeza mpango huo huku Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa, Patrick Chandi akitambua juhudi za Taasisi hiyo katika kusaidia wabunge kukabiliana na changamoto za miundombinu katika maeneo yao.

Baadhi ya wabunge walionufaika akiwemo Prof. Sospeter Muhongo, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Mgore Miraji (Musoma Mjini), Ghati Chome na Agnes Marwa wamesema msaada huo utawezesha maendeleo ya shule na vituo vya afya, vilivyopo kwenye majimbo yao.

Discussion
Reader comments
0 contributions