Skip to main content

WAATHIRIKA WA MVUA MPANDA WAOMBA MSAADA WA HARAKA KUREJESHA MAKAZI

Wakati mvua iliyoambatana na upepo mkali kunyesha na kusababisha uharibifu wa makazi na majengo katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mpanda, waathirika wa janga hilo wameiomba Serikali kutoa msaada wa haraka wa vifaa vya ujenzi ili kuwawezesha kurejesha makazi yao.

WAATHIRIKA WA MVUA MPANDA WAOMBA MSAADA WA HARAKA KUREJESHA MAKAZI
Studio Narration JAMBO FM

WAATHIRIKA WA MVUA MPANDA WAOMBA MSAADA WA HARAKA KUREJESHA...

0:00 --:--

Wakati mvua iliyoambatana na upepo mkali kunyesha na kusababisha uharibifu wa makazi na majengo katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mpanda, waathirika wa janga hilo wameiomba Serikali kutoa msaada wa haraka wa vifaa vya ujenzi ili kuwawezesha kurejesha makazi yao.

Hatua hiyo imekuja baada ya Kamati ya Maafa ya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kutembelea maeneo yaliyoathirika na kufanya tathmini ya madhara yaliyosababishwa na mvua hizo, ikiwemo nyumba kuezuliwa paa, kuta kuanguka na baadhi ya wananchi kujeruhiwa.

Akiongozana na wajumbe wa kamati hiyo, Mratibu wa Kamati ya Maafa, Boniface Kachenjela, ametembelea maeneo ya Kasokola, Uwajanja wa Ndege, Shanwe na Ilembo, ambako takribani nyumba 25 zikiwemo makazi ya wananchi, madarasa, nyumba za ibada na vyoo zimeezuliwa paa, huku baadhi ya majengo yakibomoka.

Kachenjela amesema Serikali kupitia Kamati ya Maafa imeandaa hatua za kuwasaidia waathirika, ikiwemo kuwawezesha kupata makazi ya muda, chakula na dawa, huku akiwataka wananchi kuendelea kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika.

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa viongozi wa Serikali zinaonesha kuwa madhara yameenea zaidi, ambapo Kata ya Sitalike katika Halmashauri ya Nsimbo imeripotiwa kuwa na nyumba 20 zilizobomoka, huku Mtaa wa Kilimahewa ukiwa na nyumba 17 pamoja na baadhi ya ofisi za umma zilizoathirika.

Katika Mtaa wa Migazini, Kata ya Nsemulwa, baadhi ya wananchi walioathirika wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia msaada wa vifaa vya ujenzi, wakieleza kuwa hali yao ya kiuchumi haiwaruhusu kurekebisha nyumba hizo kwa nguvu zao wenyewe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kilimahewa, Bernard Nswima, amewataka wananchi wanaoendelea kujenga nyumba kuhakikisha wanazingatia ubora wa ujenzi na usalama wa miundombinu ili kupunguza madhara wakati wa majanga.

Changamoto hii sasa inaweka hitaji la Serikali, wadau na jamii kushirikiana katika hatua mbili; msaada wa haraka kwa waathirika kurejesha makazi, pamoja na kuimarisha elimu na usimamizi wa viwango vya ujenzi ili kupunguza uwezekano wa majanga kama haya kujirudia.

Aidha, wananchi wametakiwa kuepuka kuishi katika maeneo hatarishi kama mabondeni na kando ya mito, kufukia mashimo hatarishi na kuhifadhi chakula cha kutosha, wakati mamlaka zikiendelea kufuatilia maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.