Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Ili kuchochea utalii wa ndani nchini Tanzania, wahariri , na waandishi wa habari ambao ni wanachama wa taasisi ya vyombo vya habari kusini mwa bara la Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN), walioshiriki kongamano la Taasisi ya Vyombo vya Habari lililofanyika mkoani Iringa wamepata fursa ya kufanya utalii wa ndani mkoani Iringa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa huo.
Ziara hiyo imeratibiwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na wadau wa habari mkoani humo imefanyika ikiwa ni sehemu ya siku ya pili ya kongamano la MISA TAN Summit 2026, ambapo washiriki walitembelea hifadhi mbalimbali kujionea vivutio vya utalii.

Wakiwa maeneo hayo, Makumbusho ya Chifu Mkwawa, jiwe linalozungumza la Gangilonga, lililopo eneo isimila zilipohifadhiwa zana za mawe za kale na nguzo za kale zilizojengwa kwa miamba imara pamoja na kuona hifadhi ya misitu ya SAO HILL iliyopo katika wilaya ya Mufindi mkoani humo.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo Mwenyekiti wa Misa Tanzania Edwin Soko, amesema, lengo ni kuwafanya waandishi wa habari kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii wa ndani, kwa kutumia kalamu na vyombo vya habari kuhamasisha Watanzania kutembelea maeneo ya vivutio hivyo.

Amesema Iringa ni miongoni mwa mikoa yenye fursa kubwa za utalii, zikiwemo hifadhi za taifa, mandhari ya kuvutia na urithi wa kihistoria, hivyo kuna umuhimu wa vyombo vya habari kusaidia kuvitangaza ili kuchochea uchumi wa eneo hilo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James akizungumza jana wakati wa kufungua Kongamanio hilo, amesema Iringa ni kitovu cha utalii katika Kanda ya Kusini ikiwa na vivutio vikubwa ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Udzungwa, pamoja na maeneo ya kihistoria kama Isimila na Kalenga shamba la miti "Sao Hill."

Kwa upande wao wahariri na waandishi wa habari walioshiriki wameeleza kuwa ziara hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu rasilimali za utalii zilizopo nchini, huku wakiahidi kuandika na kurusha habari zitakazohamasisha jamii kushiriki utalii wa ndani.
Kongamano la MISA TAN Summit 2026 limewakutanisha wadau wa habari, wahariri na waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini, likiwa na lengo la kujadili fursa za maendeleo pamoja na nafasi ya vyombo vya habari katika kuzitangaza.

Hatua ya MISA Tanzania kuunganisha kongamano na utalii wa ndani ni kuhamasisha watanzania kutembelea vivutio vya utalii na kwamba sekta ya utalii ni moja ya nguzo kuu za uchumi wa Taifa.
Vitutio vya utalii vingine walivyotembelea wana habari hao ni pamoja na Iringa Boma, mahali ambapo serikali ya mkoa imeanzisaha makumbusho ya kihistoria ya mkoa huo pamoja na kuangalia eneo la uwekezaji wa utalii lililotengwa na serikali mkoani kwa ajili ya kuendesha shughuli naa makongano ya kitalii.


Discussion
Reader comments
0 contributions