Skip to main content

VITA YA UHALIFU: WAMILIKI, WAFANYABIASHARA WA NYUMBA ZA KUPANGA NYAMAGANA WAPEWA TAHADHARI

Wamiliki wa nyumba za kupangisha wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza, wametakiwa kujiridhisha na historia pamoja na shughuli wanazofanya wateja wao, kabla ya kuwapangisha, ili kuzuia zisiweze kutumika na wahalifu.

VITA YA UHALIFU: WAMILIKI, WAFANYABIASHARA WA NYUMBA ZA KUPANGA NYAMAGANA  WAPEWA TAHADHARI

Wamiliki wa nyumba za kupangisha wilayani Nyamagana Mkoani Mwanza, wametakiwa kujiridhisha na historia pamoja na shughuli wanazofanya wateja wao, kabla ya kuwapangisha, ili kuzuia zisiweze kutumika na wahalifu.

​Wito huo, umetolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP. Virginia Sodoka wakati wa mkutano wa hadhara uliowakutanisha viongozi wa serikali za mitaa ya Uhuru, Rufiji na Utemini, maafisa wa Jeshi la Polisi ngazi ya mkoa na wilaya, pamoja na wananchi wa Kata za Mirongo na Mbugani.

​Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika eneo la Dampo-Pagonizi, SSP Sodoka amewataka wamiliki hao kuhakikisha wanafuata taratibu zote za kisheria za upangishaji ikiwa ni pamoja na kutambua vyanzo vya mapato vya wapangaji wao na historia ya maeneo wanayotoka.

​Amesema, "wewe baba au mama mwenye nyumba, unapangisha watu 20 au zaidi kwenye nyumba yako. Mchana kutwa wanashinda wamelala, halafu usiku wanaenda kufanya uhalifu. Ni lazima mbadilike na mjue mnaishi na watu wa namna gani."

​Aidha, SSP Sodoka aliwakumbusha wakazi na Wafanyabiashara wa kata hizo, kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama kwani jukumu la ulinzi na usalama ni la kila mwananchi na siyo Jeshi la Polisi pekee.

​Amewasihi wananchi pia kuanzisha na kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi, kwa kuwatumia vijana wazalendo, kuwapa maelekezo, mafunzo sahihi na kuwaunga mkono badala ya kuwakatisha tamaa.

​Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nyamagana, ASP Pili Saburi, alibainisha kuwa dawati hilo linapokea na kufanyia kazi kesi zote za ukatili wa kijinsia, zikiwemo za ubakaji, ulawiti na shambulio la mwili.

​Alitoa wito kwa wazazi kutotelekeza familia zao, akisisitiza kuwa malezi bora ndiyo nguzo kuu ya kujenga jamii huru isiyo na ukatili.

​"Akina baba tusitelekeze familia, akina mama tusitelekeze watoto tukaenda kuzurura, kunywa pombe na kwenda kwenye vikoba tukajisahau kurudi nyumbani kutizama watoto wetu," alisema ASP Pili.

​Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Nyamagana, ASP Mark Massawe, alitumia fursa hiyo kuwataka madereva kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za barabarani, huku akionya tabia ya baadhi ya madereva kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa pombe ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

​"Hapa mjini sheria inataka uendeshe chombo cha moto kwa kasi ya kilomita 50 au chini ya hapo kwa saa. Lakini ukishapiga kilevi chako, ukatoka hapa kwenda kule utaanguka na kupoteza maisha bure," alisema ASP Masawe.

​Mkutano huo ulihitimishwa kwa wananchi kuahidi kuunga mkono juhudi za Jeshi la Polisi za kuimarisha usalama, huku Polisi Kata ya Mirongo, Mkaguzi wa Polisi Fatuma Mpinga, akiwakumbusha wananchi kuacha kuwaogopa askari na badala yake wafike vituo vya polisi na kueleza shida zao za kiusalama.

​"Sisi tumekuja kwenu ili tujadili masuala ya kiusalama, mtutumie na msituogope. Hivi jamani tuulizane, kama hakuna amani tungeweza kukaa hapa tulipo?"

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.