Na Saada Almasi, Bariadi - Simiyu.
Maafisa Usafirishaji mjini Bariadi Mkoani Simiyu wamewataka abiria ambao wanatumia usafiri huo kuhakikisha wanatoka na dereva eneo la kituo pamoja na kukariri namba za chombo hicho ama maneno ambayo yameandikwa kwenye chombo ili kupambana na matukio ya kihalifu na tamaa ambayo yanaweza kumgharimu abiria
Rai hiyo imetolewa kufuatia mfululizo wa matukio mbalimbali ya unyang’anyi na hata vifo kwa abiria wanaotumia pikipiki hizo hapa nchini na hata wakati mwingine madereva hao kujikuta matatizoni na kuporwa pikipiki zao baada ya kubeba abiria wasio wajua ama wanaowachukua barabarani na si vituoni.
Jambo Fm imezungumza na Simon Sagula kutoka kituo cha Kidinda amesema kuwa maneno ambayo yanakuwa yameandikwa katika vyombo vyao ni utambulisho tosha kwa dereva huyo na endapo lolote linaweza kutokea mteja anaweza kurudi kijiweni na kutaja jina ili mhusika akamatwe.

“hii ni kazi kama kazi zingine na pale inapotokea changamoto kazini lazima tuimalize ili isijirudie kwa abiria ambaye hajaifahamu namba ya chombo yale majina ambayo huwa tunayaandika ni mara chache kujirudia katika kituo kimoja,kwa hiyo ukikariri tu jina ukarudi hapa hata kama amekimbia na pesa yako sisi ni rahisi kumkatama na kumchukulia hatua,” amesema Simon.
“Mwanzo tulikubaliana kwamba wakati mwingine tunapata matatizo sisi wenyewe lakini taarifa wanapozitoa watu pengine umepata ajali watu hawajui namba ni rahisi kusema pikipiki imeandikwa nini maana sisi tunajuana tutaangalia nani hayupo na kama ni wa lile jina basin i rahisi kukusaidia,” alisema Abdala Athumani.
Pamoja na tahadhari hiyo pia maafisa hao wanapiga marufuku kwa dereva ambaye si mwanachama wa kijiwe hicho kupaki kijiweni hapo ili kuondokana na mkanganyiko ambao unaweza kujitokeza

Wanasema, “kila mwanachama wa kijiwe hiki anatambulika sasa anapokuja mtu mpya ni vigumu kumruhusu kukaa hapa maana anaweza kutokea mteja akambeba kwa kuwa si mtu wa hapa akafanya tukio huko abiria atarudi hapa na kutushtaki sisi,"
"ukizingatia wakati anapaki tulimuona ni vigumu kukataa mwisho wa siku tutalazimika kumlipa yule abiria ,ndiyo maana hata iweje huwa hatumruhusu kusubiria abiria hapa labda aje na mteja wake na amsubiri huyo aondoke nae si vinginevyo,” waliongeza.
Hata hivyo jeshi la polisi kitengo cha usalama Barabarani kimekuwa kiendelea na jitihada za makusudi za kuwaelimisha maafisa hao juu ya kuchukua tahadhari za kiusalama pale wanapobeba abiria.

Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Meatu, ASP Pili Kivila anasema kuwa licha ya matukio ya unyang’anyi kutoripotiwa wilayani hapo siku za karibuni lakini jitihada bado zinaendelea kuwaelimisha maafisa hao juu ya matumizi bora ya barabara
Amesema, “utoaji wa elimu haujawahi kukoma maana kuna wale ambao wanaingia barabarani bila hata leseni ya udereva kajifunza tu kwa mtu sasa sharia za barabarani hazijui kwa hiyo kusababisha ajali ni rahisi,vilevile tunawashauri hawa abiria bora uwe na dereva ambaye unamwamini zaidi kwa safari zakoa ambaye atakuwa anakufuata ulipo ama kila unapopata safari chukua pikipiki iliyo kituoni ni ngumu sana mtu kupaki mahala ambako si pake na akaruhusiwa."
Discussion
Reader comments
0 contributions