Na Saada Almasi, Bariadi - Simiyu.
Serikali kupitia wizara ya afya inafanya jitihada katika kuendelea kuwakinga watanzania dhidi ya ugonjwa wa Malaria, ambao ni tishio hasa kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Kutokana na hilo hatua mbalimbali zimekuwa zikifanyika ikiwa ni pamoja na kugawa vyandarua vyenye dawa na kuhimiza vitumiwe ili kujikinga wao na familia zao zibaki salama.
Hivi karibuni wilaya ya Busega, Bariadi na Maswa zimepokea vyandarua zaidi ya elfu 36 vyenye dawa kwa ajili ya kugawiwa katika shule za msingi za wilaya hizo, huku msisitizo zaidi ukitolewa juu ya matumizi yake yaliyokusudiwa kutokana na vyandarua hivyo kutumika zaidi katika kuanikia dagaa wabichi na kufugia kuku badala ya kujifunika binaadamu wakati wa usiku.

Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu Prisca Kayombo akiwa katika kikao cha pamoja na viongozi wa mkoa huo amewataka viongozi hao kufikisha elimu kusudiwa kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya vyandarua hivyo.
“Hivi vyandarua havina madhara yoyote naona watu unafugia kuku,wanakaushia dagaa na kuzungushia bustani wakidai vinapunguza nguvu za kiume ,niwaombe mtusaidie kuwaambia watu wajue kuwa vimepimwa havijatufikia kama vina madhara kwa hiyo waachane na dhana potofu ili vitumike kuwalinda wao na familia zao ili tuendelee kuweka jamii salama,” amesema Prisca.

Akitoa takwimu za ugonjwa huo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dokta Yudas Ndungile amesema kuwa Malaria ni miongoni mwa magonjwa matano yanayoongoza kwa vifo na njia mojawapo ya kupambana na ugonjwa huu ni pamoja na matumizi sahihi ya vyandarua.
“Kati ya magonjwa kumi yanayoongoza nchini kwa kuua watanzania ni pamoja na Malaria ambayo inashika nafasi ya tano na watoto chini ya miaka mitano ndiyo waathirika zaidi, kwa hivyo hatari yake ni kubwa na miongoni mwa njia za kuzuia ugonjwa huu ni pamoja na matumizi sahihi ya vyandarua sasa niombe jamii nzima tupokee vyandarua hivi kwani serikali inatuthamini.” amesema Dkt. Ndungile.

Kwa upande wake Afisa kutoka Wizara ya Afya anayeshughulikia Malaria, Gitanya Peter amewasisitiza walimu ambao wamekabidhiwa vyandarua hivyo kuhakikisha kila mwanafunzi aliyeandikishwa jina amepata chandarua chake .
“isitokee mwali anamsainisha jina mwanafunzi lakini hampatii chandarua iwe ni kwa sababu yoyote umesahau au makusudi hatutotaka hilo litokee,” amesema Gitanya.
Jambo Fm imezungumza na Mwalu Rafael mkazi wa Lamadi ambaye amekiri kutumia vyandarua hivyo kuanikia dagaa akidai kuwa awali alitumia kwa sababu alisikia uvumi huo lakini baada ya kusikiliza maneno ya wataalamu amegundua hakukuwa na madhara katika vyandarua hivyo.

“Mimi nilipewa kipindi nina ujauzito nilipohudhuria kliniki lakini wenzangu wakaniambia vina madhara nikaacha kutumia kwa kulalia badala yake nikaanikia dagaa sasa kila ninavyohudhuria klinini kumpeleka mtoto madaktari wanatuambia tuachane na hayo mawazo kutokana na hilo nimemwambia hata mume wangu tunatakiwa kutumia hakuna madhara yoyote tutakayopata,” amesema Mwalu mkazi wa Lamadi.
Discussion
Reader comments
0 contributions