Na Saulo Stephen - Singida.
Maafisa wa sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wamewataka viongozi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Singida kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa mafunzo maalum yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Binto Zephania ambae ni ofisa kutoka wizara hiyo amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo viongozi hao katika masuala mbalimbali ya kisheria, utawala na usimamizi wa rasilimali za Taifa.

Amesema mada zilizotolewa katika mafunzo hayo zimejikita katika maeneo muhimu yakiwemo msaada wa kisheria, usimamizi wa rasilimali za nchi, haki na wajibu wa jamii pamoja na masuala ya ulinzi na usalama.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amesema elimu waliyoipata itasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, kuimarisha uwajibikaji na kudumisha amani pamoja na mshikamano katika jamii.

Aidha, washiriki wa mafunzo hayo walipata nafasi ya kujadili changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na namna bora ya kuzitatua kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Discussion
Reader comments
0 contributions