Na William Bundala, Kahama - Shinyanga.
Viongozi wa madhehebu ya dini wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kutumia nafasi zao katika nyumba za ibada kutoa mafundisho ya kulinda amani katika nchi ikiwa ni Pamoja na kukemea vitendo vya uhalifu katika jamii.
Wito huo, umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda katika ibada ya harambee ya ujenzi wa Kanisa la Anglikana lililopo kata Nyasubi manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

“Niwaombe sana ndugu zangu viongozi wa dini, hii nchi ni yetu sote hivyo tuna jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi wa nchi yetu ni wetu sote,tuwaombe mzidi kutoa mafundisho ya kulinda amani katika jamii,lakini pia endeleeni kukemea vitendo vya uhalifu katika jamii,” amesema Nkinda.
Nkinda pia amewataka wakazi wa Kahama kujiepusha na makundi ya mitandaoni na watu wanaokaa vijiweni kuhamasisha maandamano na kuleta vurugu na kutoa wito kwa wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao.

“Niwaombe sana wananchi wa Kahama jiepusheni na makundi ya mitandao na watu wanaokaa vijiweni bila kazi kuhamasisha maandamano na kuleta vurugu katika jamii,lakini wazazi fuatilieni mienendo ya watoto wenu, ili wale waliokengeuka muwaonye mapema,” ameongeza Nkinda.
Kwa upande wake Askofu wa Dayosisi ya Tabora, Mch. Elias Chakupewa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza serikali kwa ushirikiano mzuri na taasisi za kidini na kusema kuwa Serikali na wachungaji wote wanafanya wajibu wao wa kulea na kulinda wananchi katika misingi ya haki.

“Tunaishukuru sana na kuipongeza serikali yetu kwa ushirikiano mzuri na taasisi za kidini,sisi na wao wote tuna jukumu moja la kulea na kulinda wananchi katika misingi ya haki,Hivyo nikuhakikishie mkuu wa wilaya tutaendelea kutumia nyuma zetu za ibada kutoa mafundisho ya kulinda amani katika nchi yetu ya Tanzania,” amesema Chakupewa.
Nao baadhi ya waumini Anna Busa na Mwl. Edson Isaya wameshukuru kwa mafundisho yaliyotolewa katika ibada hiyo na kuiomba serikali kuzidi kudumisha amani kwa kutumia majeshi yote yaliyopo nchini ikiwemo jeshi la jadi la sungusungu.
“Kwakweli tunashukuru sana kwa mafundisho haya ya leo,tunaomba serikali izidi kudumisha amani katika mitaa yetu ikiwezekana hata kutumia jeshi la jadi sungusungu ilia mani na ulinzi udumishwe katika jamii.” Wamesema Waumini hao.
Harambee hiyo, ni sehemu ya jitihada za kukamilisha ujenzi wa kanisa la Anglikana Nyasubi, ambalo linatarajiwa kuhudumia waamini zaidi ya 1000 kwa wakati Mmoja.
Discussion
Reader comments
0 contributions