Skip to main content

VIKWAZO MAUZO YA PAMBA: MADIWANI WAWAKINGIA KIFUA WAKULIMA KISHAPU

Na Eunice Kanumba - Shinyanga.

VIKWAZO MAUZO YA PAMBA: MADIWANI WAWAKINGIA KIFUA WAKULIMA KISHAPU

Na Eunice Kanumba - Shinyanga.

Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, wameilalamikia Bodi ya Pamba katika Wilaya hiyo, kwa kuweka vikwazo vingi kwa Mkulima wakati akipeleka kuuza Pamba yake katika vyama vya msingi (AMCOS), jambo ambalo wamedai linamvunja moyo Mkulima kuendelea na uzalishaji wa zao hilo.

Madiwani hao wametoa kilio chao hicho katika kikao cha baraza lao,  kilichoketi katika ukumbi wa Halmashauri hiyo, ili kujadili taarifa  za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri katika kipindi cha robo ya nne  ya mwaka wa  fedha 2025/2026.

Waliowasilisha hoja hizo, ni pamoja na Diwani wa Kata ya Kishapu, Joel Ndeto na Diwani wa  Kata ya Seke, Bugolo Ferdinand Lubimbi ambapo wamesema moja wapo ya vikwazo hivyo ni pamoja kuzuia baadhi ya vyama vya msingi (AMCOS), kununua baadhi ya pamba kwa wakulima kwa madai kuwa ni chafu.

Wamesema, ili kumtia moyo mkulima kwani uzalishaji wa zao hilo ni mgumu na unapitia mchakato mwingi ni bora  bodi ya pamba ikaruhusu mkulima auze pamba yake hata kwa bei pungufu kulingana na usafi wa pamba husika kuliko michakato ya sasa  ya kuzuia AMCOS kununua pamba pamoja na upigaji wa faini,kwani unashusha morari ya uzalishaji wa zao hilo.

Akijibu malalamiko hayo katika kikao hicho mkaguzi wa pamba katika Wilaya ya Kishapu kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, Joachim Gobanya amesema, wamekuwa kusimamia   taratibu na miongozo iliyowekwa ikiwemo kutoruhusu manunuzi ya Pamba chafu, kwani baadhi ya wakulima wamekuwa wakichanganya mchanga na maji pamoja na vikonyo  katika Pamba, ili kuongeza uzito  wa pamba husika kwa kufanya udanganyifu.

“Bodi ya pamba ipo kwa mijibu wa sharia hivyo tunasimamia miongozo na taratibu zilizowekwa ikiwemo ununuaji wa pamba safi ili kulinda thamani ya zao hilo kimataifa,“ amesema Gobanya.

Akizungumzia suala hilo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Fatma Mohamed amewaasa Madiwani kwenda kutoa elimu kwa Wakulima kutochanganya Pamba na maji, mchanga na takataka zingine, kwani inachafua taswira ya zao hilo linazolishwa Nchini, katika soko la dunia.

Aidha, DAS Fatma naye amewataka  Madiwani hao kuendelea kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa wananchi, kuhusu umuhimu wa kuvuna, kuhifadhi na kusafirisha Pamba kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, ili kulinda ubora wa zao hilo.

Amesema, uhifadhi sahihi wa pamba hupunguza upotevu wa mazao, huongeza thamani ya pamba katika soko, huwapa wakulima fursa ya kupata bei nzuri na kuimarisha mchango wa zao hilo katika ukuaji wa uchumi wa Wilaya ya Kishapu na Taifa kwa ujumla.

Amewasisitiza kuendelea kushirikiana na wataalamu wa Kilimo na wadau mbalimbali, katika kuhamasisha uzalishaji wa Pamba yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.

Pamba ni moja ya mazao muhimu ya biashara nchini, hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita,  na Tabora.

Zao hilo, huchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato cha wakulima, kutoa ajira na kuingiza fedha za kigeni kupitia mauzo ya pamba na bidhaa zake katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.