Na Daniel Gahu, Mpimbwe - Katavi.
Naibu Waziri wa Fedha ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Laurent Luswetula, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwapa vijana uhuru wa kuchagua aina ya biashara wanazoamini wana uwezo wa kuzifanya, badala ya kuwaamulia shughuli za kufanya.
Luswetula amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha vijana wanatumia fursa za mitaji kwa ufanisi na kuwa na uwezo mkubwa wa kurejesha fedha wanazopatiwa.

Amesema vijana wanapopewa nafasi ya kuchagua biashara wanayoifahamu na kuamini wanaweza kuiendesha, huongeza uwezekano wa biashara hizo kustawi na kuwapatia kipato endelevu.
“Mnapowapa vijana fedha, msiwapangie biashara za kufanya. Wapeni uhuru wa kuchagua biashara wanayoijua na wanaamini wanaweza kuifanya,” amesema Luswetula.
Naibu Waziri Luswetula alitoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Usevya.

Akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Florence Chrisant, amewapongeza watumishi wa Halmashauri ya Mpimbwe kwa hatua iliyopigwa katika kipindi cha miaka 10.
Aidha, amewataka watumishi hao kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi kwa kufuatilia kero zao na kuzitatua kwa wakati, badala ya kusubiri wananchi wafike maofisini.
“Mnatakiwa kwenda kwa wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati,” amesisitiza.
Kwa upande wa wananchi, amewataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao, ili kukuza uchumi wa kaya na kuchangia maendeleo ya Mkoa wa Katavi.

Akisoma taarifa ya Halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo, Leonard Tilubuzya, amesema katika kipindi cha miaka 10 Halmashauri imepiga hatua katika kuboresha huduma za kijamii, hususan sekta ya afya.
Amesema idadi ya zahanati imeongezeka kutoka tisa mwaka 2016 hadi 15, huku vituo vya afya vikiongezeka kutoka viwili hadi sita.
Aidha, amesema Halmashauri hiyo kwa sasa ina Hospitali ya Wilaya moja, ambayo haikuwepo wakati Halmashauri ilipoanzishwa mwaka 2016.
Hatua hizo, amesema, ni sehemu ya mafanikio yaliyopatikana katika jitihada za kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi wa Mpimbwe katika muongo mmoja wa uwepo wa Halmashauri hiyo.
Maadhimisho hayo ya miaka 10 yamekuwa pia fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo na kuweka mwelekeo wa kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Mpimbwe katika miaka ijayo.
Discussion
Reader comments
0 contributions