Na Daniel Gahu - Katavi.
Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM Kata ya Kazima iliyopo Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi wameendesha semina kwa vijana wa kata hiyo ili kuchangamkia fursa mbalimbali za kimaendeleo zilizoko katika maeneo yao hususan fursa ya mikopo ya asilimia 10.
Semina hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika shule ya Sekondari Rungwa ambapo mgeni rasmi katika semina hiyo Comrade Deborah Joseph ambaye ni mjumbe wa Baraza kuu la umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi ambaye anawakilisha Mkoa wa Katavi kitaifa, amesema ni muhimu kwa vijana kupata maarifa ya kuchangamkia fursa ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

"Jambo ambalo limefanyika katika kata ya Kazima ni jambo kubwa sana wala sio dogo, ni jambo kubwa na lenye manufaa kwa mustakabali wa maendeleo kwa vijana katika kukuwa kiuchumi kwani kila mmoja kwa rika lake na umri wake amepatiwa maarifa ya namna gani ya kufanya ili aweze kufanikiwa hivyo ninawaomba sana mkazichanfamkie fursa" amesema Comrade Debora.
Amesisitiza kwa kila kijana kutambua umuhimu wa kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) kwani ndicho kigezo kikubwa na nambari moja ili mtu aweze kuwa na sifa ya kupata fursa ya mikopo ya vijana inayotolewa na Serikali kupitia wizara mbalimbali na halmashauri za wilaya.

" Kigezo kikubwa nilichokiona hapa ni NIDA na wala sio kigezo kigumu kama tunavyodhani, kwani kigezo kingine ni kufahamika kwa mtendaji wa mtaa/Kijiji na mtendaji wa Kata kitu ambacho ni rahisi kwani Serikali imewekeza pesa nyingi ili kila kijana anufaike kiuchumi" amesema Debora
Aidha amesema Mkoa wa Katavi bado unafursa nyingi sana za kiuchumi, jambo la ajabu sana vijana kutokuzikimbilia fursa hizo pindi wanapoziona kwani shughuli kama kilimo cha mbogamboga ni fursa kubwa inayopatikana ndani ya mkoa huo wa Katavi.

"Ipo mifuko ya jamii ambayo vijana wengi hawaifahamu ambapo ipo mifuko inayotoa fursa moja kwa moja kwa walengwa, ipo mifuko inayotoa dhamana pamoja na mifuko inayotoa ruzuku na programu za uwezeshaji ambapo hadi kufikia mwezi desemba kuna jumla ya mifuko ya uwezeshaji 75 ambayo itatoa fursa kwa vijana hivyo kama kijana yakupasa uchangamkie" amesema Comrade Debora.
Ameongeza kuwa mifuko iliyopo hivi sasa ya vijana, wanawake na walemavu kama ikiweza kutumiwa vizuri na vijana, basi vijana wengi wataweza kunufaika na kujikwamua kiuchumi huku akiwataka vijana wote kutembelea ofisi za Maafisa Maendeleo ya jamii ili kuweza kusaidiwa namna ya kuandika na kupangilia vyema andiko la mradi.

Akihitimisha semina hiyo amesema Mkoa wa Katavi una hali ya hewa nzuri ambao unaruhusu kufanya kila aina ya shughuli, hasa ukizingatia uwepo wa ziwa Tanganyika, Ardhi yenye rutba pamoja na maeneo makubwa ya kufanyia shughuli za ufugaji.
"Juzi nimepita pale eneo la Buzogwe nimeona gari kubwa aina ya fuso ambalo limetoka Tunduma, limeshusha shehena kubwa ya mayai na ndani ya muda mfupi mayai yale yanaisha kwa kuuzwa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Mpanda".

"Ndugu zangu sisi wa Mpanda tumeshindwa kabisa kufuga kuku wa mayai...? tufungue macho, tufungue akili, tuondoe uoga kwani vitu vya kufanya ni vingi vinavyoweza kutuinua kiuchumi" amemaliza kwa kusema Comrade Debora.
Discussion
Reader comments
0 contributions