Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Idara ya huduma ya Vijana wa Kanisa la Waadventista Wasabato, mtaa wa lubaga uliopo Manispaa ya shinyanga, wamefanya utalii wa ikolojia katika hifadhi ya msitu wa lubaga mjini hapa, kwa lengo la kujifunza masuala mbalimbali ya mazingira na asili.
Vijana hao wamefanya utalii huo ambapo mbali na masomo hayo, vijana hao pia walipata fursa ya kuburudika kwa michezo ya kubembea pamoja na kujionea wanyama aina ya ngedere wanaopatikana katika hifadhi hiyo.

Akizungumza mmoja wa vijana walioshiriki utalii huo Benjamini Martine, alisema ziara hiyo imekuwa na tija kubwa kwani imewawezesha kujifunza mambo mengi ya kiasili kwa vitendo.
"tumejifunza vitu vingi vya asili ikiwemo kuona matunda pori, miti ya dawa, namna nyuki wanavyoishi na kutengeneza asali, pamoja na mbinu bora za ufugaji nyuki ," amesema Martine.

Naye kiongozi wa idara ya huduma ya vijana wa kanisa hilo Jackson Sadick, ameeleza kuwa lengo la kuandaa utalii huo wa ndani ni kuwajenga watoto na vijana kuelewa rasilimali za asili zilizopo nchini.
Ameongeza kuwa katika ziara hiyo, wamejionea zaidi ya aina 300 za miti, ikiwamo ya sumu, matunda, na ile inayofaa kwa tiba asilia.

Kwa upande wake, msimamizi wa hifadhi ya msitu wa lubaga Wille shuli, amesema wameamua kuanzisha na kuhamasisha utalii huo wa ikolojia, ili kutoa fursa kwa wananchi na familia zao kufanya utalii wa ndani karibu na maeneo yao, huku wakipata nafasi ya kufurahi na kujifunza mambo ya kiasili.

Shuli pia ametoa wito kwa wananchi kupenda kufanya utalii wa ndani, na kwamba licha ya kupumzisha afya ya akili, pia ni kichocheo kikubwa cha uchumi wanchi.








Discussion
Reader comments
0 contributions