Na Tryphone Odace, Kasulu - Kigoma.
Vijana wametakiwa kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wa maendeleo, ili kujenga maisha yao, kujikwamua kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu katika uzinduzi wa Vijana Platform uliofanyika katika Chuo cha Ualimu Kasulu ambapo vijana walikutanishwa kwa ajili ya kujadili fursa, changamoto na namna ya kutumia nguvu na ubunifu wao katika kujiletea maendeleo.
Amewataka vijana wa Halmashauri ya Mji Kasulu, kujiandaa kwa ajili ya maisha yao ya baadaye kwa kuwa wazalendo, kufanya kazi kwa bidii na kujihusisha na shughuli zenye manufaa kwao na taifa kwa ujumla.

Katika uzinduzi huo, viongozi na wadau wameeleza umuhimu wa kuwawezesha vijana kupata taarifa sahihi, elimu, ujuzi na fursa mbalimbali zitakazowasaidia kujiajiri na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Vijana Platform inatajwa kuwa sehemu muhimu ya kuwapa vijana nafasi ya kukutana, kubadilishana mawazo na kushirikiana katika kutafuta suluhu za changamoto zinazowakabili, sambamba na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Julius Simbeye, alisema kongamano hilo limewapa vijana fursa ya kujadili changamoto zinazowakabili, kubadilishana uzoefu pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto hizo.

"Tuko hapa kubadilishana mawazo na kupeana taarifa sahihi katika hali tunazopitia sisi kama vijana na naamini mkiwa hapa mtapokea mawazo mapya na sisi kama serikali tuseme milango ipo wazi kupokea mawazo ya vijana na kuwasaidia kufikia wanapohitaji kufika kwa mfano mkiunda vikundi mkaja kwetu tunawapa mikopo kikubwa uwe na wazo tunawapa pesa mbajikwamua kiuchumi" alisema Simbeye
Naye Amina Kaniki kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, aliwataka vijana kutumia teknolojia na fursa za kidijitali ili kupata taarifa kuhusu fursa zilizopo katika maeneo yao na kuzitumia katika kujiletea maendeleo na kulisaidia taifa kupiga hatua.

"Jitahidi kuendana na kasi ya digitali kuna fursa huko kwa kupata taarifa sahihi ili ziwasaidie kufikia malengo ya kile mnachotaka," alisema Kaniki.
Hata hivyo baadhi ya vijana walioshiriki katika kongamano hilo walisema wamefahamu fursa zilizopo katika maeneo yao na kupata nafasi ya kubadilishana uzoefu ambao utawasaidia katika kujenga maisha yao.
Kongamano hilo limehudhuriwa na zaidi ya vijana 1,300 kutoka maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji Kasulu na uzinduzi huo umefanyika ukiwa na ujumbe wa kuwataka vijana kuwa sehemu ya mabadiliko na maendeleo ya jamii, kwa kutumia vipaji, maarifa na nguvu walizonazo.
Discussion
Reader comments
0 contributions