Skip to main content

VIJANA MSILALAMIKE, TUMIENI FUSRA ZILIZOPO KUJIKWAMUA KIUCHUMI - MSIGWA

Na Gideon Gregory - Dodoma.

VIJANA MSILALAMIKE, TUMIENI FUSRA ZILIZOPO  KUJIKWAMUA KIUCHUMI - MSIGWA

Na Gideon Gregory - Dodoma.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewataka vijana nchini kutumia fursa zilizowekwa na Serikali kujikwamua kiuchumi badala ya kujihusisha na vitendo vya vurugu na maandamano.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi katika Soko la Wafanyabiashara Wadogo (Machinga Complex ) jijini Dodoma leo Julai 22,2026 Msigwa amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa masoko na miundombinu wezeshi ili kuwapa vijana mazingira bora ya kufanya biashara na kujipatia kipato.

"Vijana fursa zipo, haitoshi kubaki tunalalamika hali ya uchumi, tujikusanye kwenye masoko kutafuta pesa, siyo barabarani kufanya fujo, maeneo ya masokoni ni maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya vijana kujiongezea kipato na kujenga maisha yao,"amesema.

Aidha, amesema Serikali imeongeza kiwango cha fedha zinazotengwa na halmashauri kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 ya mapato ya ndani, ambapo asilimia 10 itaendelea kutolewa kwa vijana, huku sehemu nyingine ikielekezwa kwa wanawake, makundi maalumu na ujenzi wa miundombinu wezeshi kama masoko na maeneo ya biashara.

"Asilimia tano ya nyongeza itaelekezwa katika kujenga miundombinu wezeshi ikiwemo masoko na maeneo mengine yatakayowawezesha vijana kufanya biashara na kuongeza kipato chao,"amesema.

Katika hatua nyingine Msigwa amewataka vijana kutowaruhusu watu kuwashawishi kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na maendeleo yao, akisisitiza kuwa njia sahihi ya kujenga maisha ni kufanya kazi, kufanya biashara na kutumia fursa zinazotolewa na Serikali.

"Msikubali kushawishiwa kufanya fujo ambazo haziwapi kipato. Wasikilizeni wanaowaelekeza kutafuta pesa, kwenda sokoni, kulima na kufanya biashara. Serikali ipo tayari kushirikiana na vijana kuhakikisha wanainua uchumi wao,"amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dodoma, Christian Msumari amesema ujenzi wa soko hilo umebadili maisha ya wafanyabiashara kwa kuwapatia sehemu salama za biashara na kuwawezesha kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.

Nao baadhi ya wafanyabiashara katika soko hilo la Machinga Complex akiwemo Rahma Iddi na Bakari Salimu wameiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya masoko ili wafanyabiashara wadogo wafanye kazi kwa utulivu na kuongeza kipato chao.

Ziara ya Msemaji wa serikali katika soko la Machinga Comlex Dodoma imelenga kuwasisitiza vijana kuwekeza nguvu katika kutafuta Fedha Kwenye masoko ili kuongeza kipato chao na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.