Vifaa 14 vyenye thamani ya shilingi milioni 55,560,000. vimetolewa kwa wakulima kutoka Halmashauri za Kasulu, Kibondo na Kakonko kutoka shirika la world Vision Tanzania kwa lengo kuongeza uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani katika mazao ya chakula na biashara
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Mratibu wa miradi ya World vision Wilayani Kakonko, Fadhili Nicodemus alisema lengo la mpango huo ni kuendeleza mawazo ya wakulima ili kuwasaidia kutoka katika kilimo cha mazoea na kujikita katika kilimo chenye tija.

Akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia uchumi na uzalishaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma James Peter, aliwapongeza wadau wa maendeleo waliofanikisha upatikanaji wa vifaa hivyo, huku akiwataka wakulima hao kutumia vitu hivyo ili viweze kuleta manufaa kwao.
Alisema mashirika ya World Vision Tanzania na Good Neighbors kupitia mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI), unaofadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini kupitia Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), wamekabidhi vifaa hivyo baada ya washindi wa andiko bora la mradi wa kilimo biashara kupiwa na kukidhi matakwa ya mradi wenye lengo la kuwasaidia kuboresha shughuli za kilimo.

Naye Mkuu wa ofisi ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Wilayani Kasulu, Daniel Dynel amesema vifaa walivyovipata wavitumie vizuri ili kuongeza uchumi wao kupitia shughili za kilimo.
Amesema kuwa mradi huo unalenga kuhakikisha unawainua wakulima kupitia shughuli za kilimo chenye tija na kiweze kuwanufaisha kibishara katika masoko ya ndani na nje ya nchi

Kwa upande wake, Afisa maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kakonko, Mustapha Mtungwa, amewataka wakulima kuzitumia mashine hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kufanikisha malengo ya mradi.
Baadhi ya wakulima walionufaika na mradi huo waliwashukuru wadau wa maendeleo kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vinakwenda kurahisisha katika shughuli zao za kilimo.

Makabidhiano hayo ni awamu ya pili ya utoaji wa mashine na vifaa vya kilimo kwa wakulima wa wilaya za Kakonko, Kibondo na Kasulu ambapo katika awamu hii, vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mashine 10 za kusagia nafaka, mashine mbili za kupukuchulia mahindi na pampu mbili za maji zinazotumia jenereta.
Discussion
Reader comments
0 contributions