Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Singida umeanza Wiki ya UWT kwa kutembelea Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba, Kiomboi, na kutoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo sabuni na mafuta kwa ajili ya kuwasaidia kina mama wanaopatiwa huduma hospitalini.
Zoezi hilo limeongozwa na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Singida, Martha Kayaga, akiambatana na Mbunge wa Viti Maalum, pamoja na viongozi na wanachama wa UWT Mkoa wa Singida, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mshikamano na kuwajali wanawake pamoja na familia zinazopitia kipindi cha kujifungua.
Kutoka kushoto Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Singida Martha Kayaga, anayefuata ni Mama aliyejifungua Pacha wawili,akifuatiwa na Mbunge wa Viti Maalumu Grace Mkomwa na mwisho kulia ni Katibu wa UWT Mkoa Singida Judith Mwamboza
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Martha Kayaga amesema UWT itaendelea kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali, hususan zinazowakabili wanawake na watoto, huku akisisitiza umuhimu wa wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Singida Grace Mkomwa akiwa kwenye wodi ya wazazi hospitali ya Wilaya ya Iramba Kiomboi
Wiki ya UWT imeanza rasmi Septemba 28, 2026, ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazolenga kuimarisha nafasi ya wanawake katika jamii na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo.
Discussion
Reader comments
0 contributions