Na Saulo Stephen - Singida.
Serikali imesema itaendelea kuwajengea uwezo vijana katika ujasiriamali, usimamizi wa fedha, biashara na ujuzi wa kazi ili kuongeza uwezo wao wa kujitegemea na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia programu za uwezeshaji wa vijana kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya mkopo wa shilingi milioni 263 kwa kikundi cha vijana kinachoendesha shughuli za kiwanda cha ukamuaji mafuta ya alizeti kilichopo kijiji cha Makunda Wilaya ya Iramba pamoja, ikiwa ni pamoja na mkopo wa shilingi milioni 100 kwa kikundi cha Mama Lishe wa Manispaa ya Singida na kufanya jumla ya shilingi milioni 363.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Makundi, Agosti 17,2026 ,Serikali pia ilikabidhi gari la kubeba mazao ya alizeti litakalotumika kusafirisha mazao kutoka mashambani hadi kiwandani, hatua inayotarajiwa kurahisisha upatikanaji wa malighafi na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Waziri Nanauka amebainisha kuwa uwezeshaji wa vijana hauishii kwenye utoaji wa mitaji pekee, bali unaenda sambamba na kuwapa maarifa yatakayowawezesha kusimamia biashara zao kwa ufanisi na kuhakikisha zinakuwa endelevu.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amesema, viwanda vidogo vinavyojikita katika uchakataji wa alizeti vimekuwa chanzo muhimu cha ajira kwa vijana wengi, huku shughuli za ukamuaji wa mafuta zikitoa fursa ya kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wao, wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuwawezesha, wakiahidi kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa pamoja na kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwapa nafasi vijana wengine kunufaika na programu hiyo.

Discussion
Reader comments
0 contributions