Na Afarah Suleiman, Mbulu - Manyara.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Maryam Muhaji ameagiza kuongezwa kwa mafundi katika miradi ya maendeleo akibainisha kuwa uhaba wa wataalamu hao ni miongoni mwa sababu kuu zinazochelewesha kukamilika kwa miradi hiyo.
Ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa miradi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu, ambapo alikagua ujenzi wa jengo la utawala pamoja na jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Halmashauri hiyo.

Muhaji amesema kuongeza idadi ya mafundi kutaharakisha utekelezaji wa miradi na kuwezesha kukamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma zinazolengwa.
“Ongezeni mafundi katika miradi ili kuharakisha kasi ya utekelezaji wananchi waanze kupata huduma bora katika majengo haya" amesema Muhaji.

Aidha, amesisitiza kuwa pamoja na kuongeza mafundi, ni muhimu kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana kwa wakati ili kuepusha kusuasua kwa kazi.
Amesema, Serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii, hivyo ni wajibu wa wasimamizi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Rehema Bwasi ameahidi kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Discussion
Reader comments
0 contributions