Na Faustine Kasala - Kigoma.
Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Kasulu vijijini vimetajwa kuwa vinara wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya wilaya hizo Mkoani Kigoma katika mwaka wa fedha 2024-2025 hadi sasa jambo ambalo limechagizwa na usimamizi mathubuti wa watumishi wa Idara mbalimbali wa Halmashauri hizo katika ukusanyaji wa mapato ya ndani
akizungumza na wananchi pamoja na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema Halmashauri zote kwa ujumla zinatakiwa kuendelea kusimamia kwa ufanisi zoezi la ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza mapato na kufikia malengo endelevu ya mkoa huo.

"Ongezeko la mapato ya ndani litaziwezesha halmashauri kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kutenga fedha kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 hatua itakayosaidia wananchi kujikwamua kiuchumi hivyo nawaomba sana watumishi wote kila mmoja kwa nafasi yake simamieni kwa ufanisi zoezi hili," alisema Rugwa.
Aidha Rugwa amesema Mkoa wa Kigoma katika mwaka wa fedha 2024-2025 hadi sasa Mkoa umeshuhudia mafanikio makubwa katika utengaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya makundi ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu kwa Halmashauri zote.

"Kiasi cha fedha kinachopelekwa kutoka kwenye Halmashauri kimeendelea kuongezeka na hata mapato yetu yameongezeka mpaka tunamaliza 2024-2025 tumefanikiwa kukusanya kiasi cha zaidi ya Tshl Billion 25 na mwaka huu tumekusudia kukusanya zaidi ya Tshl Billion 29 na niseme tu kwamba Halmashauri ambazo zimekuwa kinara katika ukusanyaji wa mapato ni Kasulu Dc na Uvinza," alisema Rugwa.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kasulu wamesema halmashauri zinapaswa kuongeza umakini katika ukusanyaji wa mapato hususani maeneo ya vijijini ili kuongeza ufanisi wa mapato na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Discussion
Reader comments
0 contributions