Skip to main content

UVAMIZI MAENEO YALIYOTENGWA KWA MATUMIZI MAALUM UNARUDISHA NYUMA MAENDELEO - RC MRINDOKO

Na Daniel Gahu - Katavi.

UVAMIZI MAENEO YALIYOTENGWA KWA MATUMIZI MAALUM UNARUDISHA NYUMA MAENDELEO - RC MRINDOKO

Na Daniel Gahu - Katavi.

Mipango na mikakati ya Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo mara kadhaa hukwamishwa na migogoro inayoibuka hususan katika maeneo yaliyotengwa.

Jambo hilo limemuibua Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko kwa kulipongeza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambalo limefanya uamuzi wa haraka wa kutenga eneo maalumu kwa ajili ya Maonesho ya Nanenane, akisema hatua hiyo ni ya kimkakati katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani Katavi.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika viwanja vya Nanenane vya Mizengo Pinda vilivyopo Kata ya Kabungu, Mrindoko amejionea hali ya maendeleo na fursa zilizopo katika eneo hilo.

Amesema, baadhi ya watu wamekuwa wakivamia maeneo yaliyotengwa kwa matumizi maalumu na kuyauza kwa wananchi kinyume cha sheria, jambo linalohatarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

"Uvamizi wa maeneo yaliyotengwa kwa matumizi maalumu unarudisha nyuma jitihada za Serikali za kuleta maendeleo na kuathiri mipango ya uwekezaji inayolenga kuinua uchumi wa wananchi," amesema RC Mrindoko.

Aidha, amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kuhakikisha kuanzia mwezi Juni, taasisi na wadau wote waliopatiwa maeneo katika viwanja hivyo wanaoneshwa rasmi maeneo yao na kuanza uwekezaji mara moja ili kuongeza tija ya matumizi ya ardhi.

Pia, amewahimiza wananchi wa Kabungu na Wilaya ya Tanganyika kutumia fursa zitakazotokana na uwepo wa viwanja hivyo vya maonesho kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi. Sambamba na hilo, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kutenga eneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogowadogo ili waweze kunufaika na fursa za biashara zitakazojitokeza.

Amesema, viwanja hivyo vinatarajiwa kuanza kutumika rasmi kwa Maonesho ya Nanenane yatakayofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa anayesimamia Uchumi na Uzalishaji, Nehemia James amesema, maandalizi yanaendelea ambapo shughuli za usafishaji wa eneo, usafishaji wa barabara za ndani na uondoaji wa vichaka zinafanyika kabla ya kuanza hatua ya upangaji wa ramani, itakayoonesha mpangilio wa mabanda na maeneo mbalimbali ya maonesho.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.