Baadhi ya wananchi mkoani Mara wameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa uchumi, ikiwemo ujenzi wa barabara, madaraja na miundombinu ya elimu.
Pongezi hizo zimetolewa wakati Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara ilipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Ametaja ujenzi wa daraja katika Mto Tigite kuwa miongoni mwa miradi iliyokuwa na umuhimu mkubwa kutokana na changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili wananchi wakati wa kuvuka mto huo na wakati mwingine kuwalazimu kuvuka kwa kamba.

Kamati hiyo pia imetembelea miradi ya elimu ikiwemo Shule ya Sekondari Matongo na Shule ya Sekondari Mjini Kati Nyamongo, ambapo viongozi wamekagua maendeleo ya miundombinu inayoendelea kujengwa katika shule hizo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime,Meja Edward Gowele, pamoja na viongozi wa CCM wamesema wataendelea kusimamia kwa karibu miradi yote ya serikali ili ikamilike kwa wakati na kuleta tija kwa jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa wilaya ya Tarime wamesema miradi inayotekelezwa imechangia kurahisisha usafiri na usafirishaji, kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu katika maeneo yao.
Discussion
Reader comments
0 contributions