Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amezitaka timu za wataalamu zinazohusika na utatuzi wa migogoro kuhakikisha zinashughulikia kero za wananchi, kwa kuzingatia haki na kufuata taratibu ili kupata suluhisho la kudumu.
Mtatiro ametoa maagizo hayo , wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Tarafa ya Itwangi, uliofanyika katika Shule ya Msingi Didia, iliyopo wilayani Shinyanga.

Amesema, kero zote zilizowasilishwa katika mkutano huo zinapaswa kushughulikiwa ndani ya siku 14 na kwamba wataalamu watakaopewa jukumu hilo wanapaswa kufanya kazi kwa umakini, weledi na kwa misingi ya haki.
“Mnapotatua migogoro ya wananchi, katendeni haki. nimeshawahi kutuma timu za halmashauri kwenda kutatua mgogoro, lakini ziliponiletea taarifa nikakataa kwa sababu hazikuwa zimetenda haki, nilifika mwenyewe eneo husika na kutatua mgogoro huo tofauti na walivyopendekeza, na hadi leo wananchi wanaishi kwa utulivu,” amesema Mtatiro.

Aidha, ameagiza pia katika utatuzi huo wa kero za wananchi, timu za wataalamu, wafike kwenye maeneo husika ya wananchi na utatuzi huo ufanyike pia kwa maandishi.
Katika mkutano huo, wananchi pamoja na Wenyeviti wa vijiji akiwamo Kulwa Masesa, waliwasilisha kero mbalimbali zikiwamo migogoro ya ardhi na mipaka, masuala ya mirathi, ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa huduma za maji safi na salama pamoja na changamoto za upatikanaji wa umeme.

Mtatiro ameahidi kuwa, serikali ya wilaya itaendelea kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo ili kuhakikisha wananchi wanapata haki na huduma bora kwa wakati.


Discussion
Reader comments
0 contributions