Chanzo rasmi cha ajali ya ndege iliyoua watu tisa Florida bado hakijatolewa. Mamlaka za usafiri wa anga nchini Marekani zimesema uchunguzi bado unaendelea.
Kwa mujibu wa taarifa ya awali kutoka Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) na Shirika la Usafiri wa Anga (FAA), ndege aina ya Learjet 60 yenye namba ya usajili N722BD ilikuwa katika urefu wa futi 35,000 ikitoka Austin, Texas kuelekea Bahamas.
Mawasiliano ya mwisho kati ya rubani na kituo cha kudhibiti anga (ATC) yanaonesha rubani aliripoti changamoto kadhaa. Alidai kuna barafu iliyokuwa inaganda kwenye ndege (icing), mtikisiko wa wastani (turbulence) pamoja na mvua kubwa.

Baada ya taarifa hiyo, hali ilibadilika ghafla. Ndege ilianza kushuka kwa kasi ya ajabu. Data za safari zinaonesha iliporomoka kwa futi takriban 27,000 ndani ya dakika moja tu, huku taarifa nyingine zikieleza kushuka kwa futi hadi 32,000 kwa dakika.
Katika muda huo, rubani alitangaza dharura (Mayday) na kuripoti tatizo la overspeed, maana yake ndege ilizidi mwendo wa juu unaoruhusiwa wa Mach 0.81 hadi karibu Mach 0.90, na kudunda kwa pua karibu wima.
Mpaka sasa sababu halisi ya kuanguka bado ni nadharia. Wataalamu wa anga wanaangalia uwezekano wa mambo matatu makuu.
1. Barafu kwenye Mkia wa Ndege:
Barafu inaweza kusababisha tailplane stall na kuifanya pua ya ndege kudunda ghafla bila rubani kuweza kuirudisha.

2. Mach tuck.
Kwa mwendo mkubwa sana mawimbi ya hewa kwenye mabawa husababisha ndege kudunda yenyewe na nguvu za upepo kuibamiza.
3. Hali ya hewa.
Ilielezwa kuwa, kulikuwa na dhoruba kali Florida siku hiyo, ingawa FAA bado haijaunganisha moja kwa moja hali ya hewa na ajali.
Wakati ndege hiyo ilipogonga eneo la Military Trail na 10th Avenue North karibu na Greenacres, iliacha shimo kubwa barabarani na kulipua bomba la maji, na kusababisha watu takriban 600 kuhamishwa kwenye makazi ya jirani.
NTSB imeweka timu maalum katika eneo la tukio tangu Jumapili na inatarajiwa kutoa taarifa ya awali leo Jumatatu huko West Palm Beach. Ripoti kamili inatarajiwa kuchukua miezi kadhaa.
Kwa sasa majina ya abiria tisa waliofariki hayajatajwa rasmi, ingawa Mamlaka zimesema zinasubiri familia zote zitaarifiwe kwanza.
Discussion
Reader comments
0 contributions