Skip to main content

USHIRIKIANO KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO TABORA UNACHOCHEA MAENDELEO YA KIJAMII - BI. UPENDO

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Bi. Upendo Rweyemamu, amelipongeza shirika la BRAC International kwa ushirikiano wake na Mastercard Foundation katika kutekeleza Mradi wa Uwezeshaji wa Mabinti na Wanawake Vijana, akieleza kuwa mpango huo una mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

USHIRIKIANO KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO TABORA UNACHOCHEA MAENDELEO YA KIJAMII - BI. UPENDO

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Bi. Upendo Rweyemamu, amelipongeza shirika la BRAC International kwa ushirikiano wake na Mastercard Foundation katika kutekeleza Mradi wa Uwezeshaji wa Mabinti na Wanawake Vijana, akieleza kuwa mpango huo una mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha wadau wa mradi huo kilichofanyika mkoani Tabora, Bi. Rweyemamu amesema kuwa kupitia mafunzo mbalimbali yanayotolewa, mabinti na wanawake vijana wamekuwa wakipata ujuzi wa maisha, maarifa ya ujasiriamali pamoja na uwezo wa kutambua na kutumia fursa za kiuchumi zinazowazunguka.

Amebainisha kuwa elimu hiyo imechangia kuwasaidia walengwa wengi kukabiliana na changamoto za kijamii, ikiwemo hatari ya kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya kutokana na ukosefu wa stadi muhimu za maisha.

“Tunathamini mchango wa BRAC katika kuwajengea uwezo vijana wetu wa kike. Mafunzo haya yamewapa maarifa, kujiamini na mwelekeo bora wa maisha, hivyo kuwasaidia kuepuka vishawishi na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri mustakabali wao,” amesema Bi. Rweyemamu.

Aidha, amewataka wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali ili kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili walengwa wa miradi ya uwezeshaji, hususan upatikanaji wa mitaji, masoko na elimu ya biashara, ili kuhakikisha manufaa ya miradi hiyo yanawafikia wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Uwezeshaji wa Mabinti na Wanawake Vijana Mkoa wa Tabora, Bw. Isihaka Mirambo, amesema mradi huo unatekelezwa katika zaidi ya mikoa 10 nchini kwa ufadhili wa Mastercard Foundation kupitia BRAC International.

Ameeleza kuwa mradi huo ulianza mwaka 2021 na unatarajiwa kuendelea hadi mwaka 2030, ukiwalenga mabinti na wanawake vijana wenye umri kati ya miaka 12 na 35 kupitia afua za elimu, uwezeshaji wa kijamii na maendeleo ya kiuchumi.

Naye mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Gulamhussein Dewji, amesisitiza kuwa viongozi wa Serikali za Mitaa wataendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi wa Tabora.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.