Skip to main content

USHETU YAFIKA TANGANYIKA DC KUCHOTA UZOEFU KILIMO CHA TUMBAKU, BIASHARA YA KABONI

Viongozi, madiwani na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Hadija Mohamed Kabojela, wameitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu uendeshaji wa kilimo cha tumbaku na pamba, usimamizi wa mikataba ya kilimo pamoja na utekelezaji wa biashara ya kaboni.

USHETU YAFIKA TANGANYIKA DC KUCHOTA UZOEFU KILIMO CHA TUMBAKU, BIASHARA YA KABONI
Studio Narration JAMBO FM

USHETU YAFIKA TANGANYIKA DC KUCHOTA UZOEFU KILIMO CHA TUMBAK...

0:00 --:--

Viongozi, madiwani na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Hadija Mohamed Kabojela, wameitembelea Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu uendeshaji wa kilimo cha tumbaku na pamba, usimamizi wa mikataba ya kilimo pamoja na utekelezaji wa biashara ya kaboni.

Katika ziara hiyo, ujumbe huo umejifunza mifumo ya usimamizi wa mikataba kati ya wakulima, vyama vya ushirika na kampuni za tumbaku, pamoja na mikakati ya kuimarisha uwazi na kulinda maslahi ya wakulima. Mikakati hiyo inajumuisha ukaguzi wa mara kwa mara na maalumu, kuimarisha timu za ufuatiliaji kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama ya Wilaya, na kuweka utaratibu madhubuti wa usimamizi wa mikataba.

Aidha, madiwani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu wamevutiwa na namna Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika inavyosimamia na kutekeleza biashara ya kaboni. Wameeleza nia ya kutumia uzoefu na maarifa waliyoyapata kuimarisha usimamizi wa mazingira na kuendeleza biashara hiyo katika Halmashauri yao, ili wananchi nao waweze kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na uhifadhi wa misitu na mazingira.

Vilevile, ujumbe huo umetembelea viwanja vya maonesho vya Nanenane, Kabungu, kujionea maandalizi ya Wiki ya Mwanakatavi, kufuatia mwaliko wa Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Mhe. Onesmo Buswelu. Maonesho hayo yanatarajiwa kuanza tarehe 25 Oktoba 2026, yakilenga kuwakutanisha wakulima, kampuni za pembejeo na zana za kilimo, wajasiriamali pamoja na wadau wa sekta binafsi.

Maonesho hayo yatatoa fursa ya kujifunza teknolojia na mbinu bora za kilimo, kutangaza bidhaa na huduma, pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa maendeleo. Ziara hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano baina ya halmashauri katika kubadilishana uzoefu, kubuni mikakati ya maendeleo na kutumia fursa zilizopo kuinua uchumi wa wananchi.

Kupitia ziara hiyo, wajumbe na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu walipata elimu kuhusu biashara ya hewa ukaa, ambayo inahusisha juhudi za kulinda na kuhifadhi misitu pamoja na rasilimali nyingine za asili ili kuchangia kupunguza ongezeko la hewa ukaa katika anga. Shughuli hiyo pia inatoa fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoshiriki katika uhifadhi wa mazingira.

Aidha, ilielezwa kuwa biashara ya hewa ukaa inaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa Halmashauri na wananchi, hivyo kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kuboresha huduma za kijamii na kuongeza fursa za kiuchumi katika jamii.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imeeleza kuwa imefanikiwa kukusanya takribani shilingi bilioni 30 kupitia biashara ya hewa ukaa, jambo linaloonesha uwezekano wa kutumia rasilimali za asili kwa njia endelevu ili kuongeza mapato na kuchochea maendeleo.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu za kujifunza na kubadilishana uzoefu na Halmashauri nyingine nchini, kwa lengo la kubaini fursa mpya za kuongeza mapato ya ndani, kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.