Na Ibrahim Rojala - Geita.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa na Mbunge, Mary Chatanda, amesema wanawake nchini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa usawa wa kijinsia, ukatili wa kijinsia pamoja na kukosa fursa sawa katika maeneo ya kazi.
Chatanda ameyasema hayo kupitia hotuba yake katika Tamasha la Mwanamke wa Dhahabu (Geita Women Festival 2026) lililofanyika Juni 6, 2026 katika ukumbi wa Golden Social Hall, Manispaa ya Geita.

Katika hotuba hiyo, Chatanda alitoa wito kwa jamii kuimarisha ushirikiano katika malezi ya watoto, akisisitiza kuwa maadili mema ni urithi mkubwa kwa watoto na yatawasaidia kukabiliana na mmomonyoko wa maadili pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, aliwashukuru waandaaji wa tamasha hilo na kutumia fursa hiyo kumpongeza Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake katika kuwawezesha wanawake mkoani Geita.

Shigela alisema, miongoni mwa mafanikio hayo ni upatikanaji wa leseni 30 za uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa vikundi vinavyojumuisha wanawake wapatao 900, hatua ambayo imechangia kuwawezesha kiuchumi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini,Mhandisi Chacha Mwita Wambura, alimpongeza Mkurugenzi wa Shirika la Geita Women and Youth Foundation, Cecylia Miraji, kwa kufanikisha tamasha hilo lililolenga kutambua na kuwatunuku wanawake vinara katika sekta mbalimbali za maendeleo mkoani Geita.

“Kipekee sana nimpongeze mwandaaji, dada yetu Cecy, kwa jinsi alivyoandaa Geita Women Festival ambayo imeleta hamasa kubwa kwa wanawake. Tukio hili limewatia moyo, limewajengea kujiamini na kuwahamasisha kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo,” alisema Wambura.
Naye Cecylia Miraji alisema kuwa tamasha hilo limeandaliwa kwa lengo la kutambua na kuthamini wanawake wenye mchango mkubwa katika jamii kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo.

Alisema mafanikio ya wanawake wengi yanathibitisha kuwa mwanamke akipewa fursa, elimu na mazingira rafiki ana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Tamasha hili limelenga kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwainua wanawake kiuchumi na kijamii. Tunaamini maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana kwa kasi inayotakiwa bila ushiriki wa wanawake,” alisema Miraji.

Katika utoaji wa tuzo hizo, mshindi wa Tuzo ya Mwanamke Mchimbaji Bora wa Madini ya Dhahabu Mkoa wa Geita, Salma Mipawa, alitoa wito wa kuendelea kuwapa wanawake nafasi zaidi za kushiriki katika shughuli za kiuchumi na maendeleo.
Kwa upande wake, Zubeda Handrish, aliyeshinda Tuzo ya Mwandishi Bora wa Habari, alisisitiza umuhimu wa waandishi na watendaji wengine kuzingatia maadili ya kazi ili kujenga jamii yenye uwajibikaji na maendeleo endelevu.
Discussion
Reader comments
0 contributions